The House of Favourite Newspapers

WANNE WA FAMILIA MOJA WAPOFUKA KIMA AJABU!

DAR ES SALAAM: Hujafa hujaumbika! Ndugu wanne wa familia moja wamejikuta wakiteseka baada ya kupata tatizo la kupofuka macho bila kujulikana kiini cha tatizo hilo.  Wiki mbili zilizopita, ndugu hao; Furahini Kassian (kaka mtu), Lenata Lukesi (mama) na Elimina Lukasi (bibi) walifika Chanika jijini Dar, kwa ajili ya kuomba msaada kwa Watanzania.

 

Akizungumza na Risasi Jumamosi, mtoto pekee ambaye amenusurika kupata ulemavu huo wa macho, Mwambagi Yusuph (18) alisema kuwa yeye na familia yake wanaishi Kijiji cha Tunke, Tarafa ya Turiani Mkoani Morogoro lakini wamelazika kuja Chanika kuomba msaada katika makanisa mbalimbali.

 

“Tulielekezwa huku Dar tuje kwa ndugu wa jirani yetu wa kule Morogoro tuje kuomba msaada katika makanisa hivyo tukafika lakini bahati mbaya bado hatujapata msaada wa kujikimu,” alisema binti huyo.

 

Akizidi kusimulia kwa uchungu huku machozi yakimlengalenga, msichana huyo alisema kwa sasa yeye anasoma kidato cha nne lakini kutokana na familia yake kuwa na maisha duni, analazimika kufanya vibarua mbalimbali kila anapotoka shule ili kupata fedha za kujikimu kimaisha maana ni yeye pekee wanayemtegemea kwani ndiye anayeona kwenye familia yake.

 

“Kwa kweli napitia kipindi kigumu sana mpaka kuna wakati najiuliza maswali mengi na sipati majibu maana mimi ndio mdogo lakini familia yote inanitegemea mimi kwa kila kitu. Mimi mwenyewe nahitaji msaada ili niweze angalau kumaliza shule hata nije kusaidia familia yangu,” alisema binti huyo. Akiendelea kuzungumzia historia ya ugonjwa huo wa upofu kwa ndugu zake, msichana huyo alisema tatizo hilo limeitafuna familia kuanzia kwa marehemu baba yake Yusuph Kassian.

 

Alisema baba yake alifariki dunia mwaka 2004 ambapo naye alikuwa na tatizo la kupofuka macho lakini cha kusikitisha zaidi, mama yake pia alikuwa mzima tu baada ya kuwazaa yeye na kaka yake macho yake yakaanza kupoteza uwezo wa kuona mpaka akawa kipofu kabisa. Alisema na kaka yake huyo naye alikuwa mzima, macho yakaanza kumuuma kwa muda mrefu na hatimaye naye akapata upofu na hata bibi yake mzaa mama (Elimina Lukasi) wanayeishi naye pia alipata tatizo hilo.

 

“Walihangaika katika hospitali mbalimbali Morogoro na Dar lakini kote ilishindikana na haijulikani kimsingi wana tatizo gani. Kama mtoto wa kike napitia kipindi kigumu sana, watu wengi wananitishia amani hasa wanaume ambapo wengi wananitongoza, nikikataa wanatishia kunibaka wanasema siwezi kuwafanya kitu kwa sababu wazazi wangu na ndugu zangu hawaoni,” alisema Mwambagi.

 

Mbali na hilo, binti huyo alisema, nyumba wanayoishi inasikitisha kwa sababu ni ya udongo na tayari imebomoka upande mmoja na hapo si yao bali kuna mtu aliwapa kuwahifadhi tu.

 

Mwambagi na familia yake ambao wanatarajia kurudi nyumbani kwao Morogoro muda wowote, wanapitia katika mazingira magumu yeye na familia yake na wanahitaji msaada wa hali na mali ili kujikwamua kimaisha. Endapo umeguswa na habari hii unaweza kuwachangia chochote kupitia simu yao ya mkononi 0712625476. Kumbuka kutoa ni moyo na si utajiri!

Tuwasaidie ndugu zetu hawa ili nao wayafurahie maisha-Mhariri.

STORI: Imelda Mtema, Risasi Jumamosi

Comments are closed.