The House of Favourite Newspapers

Waoo…! Kama Jana Vile!-15

0

ILIPOISHIA RISASI JUMATANO:

“Sasa hapa si anaagwa tu, hata kama alikufa kwa ngoma ni vilevile, anaagwa.”

“Kwa hiyo mama Monica unaamini mimi nina ngoma na nimekuambukiza wewe?”

“Ndiyo. Kama si kweli twende sasa hivi tukapime hospitali ili niamini,” alisema mama Monica na kuanza kulia.

JIACHIE MWENYEWE…

 

Magembe alijifikiria kwa muda kisha akamwangalia mama Monica kwa macho yenye maswali kibao…

“Baby, ina maana kweli kabisa huniamini sasa kwa sababu ya maneno ya uongo ya yule kijana?”

“Ndiyo, maelezo yako si sahihi Magembe. Yaani umepanga kuniangamiza hivihivi…twende sasa hivi tukapime mimi nipo tayari.”

Magembe alijiinamia, akahema kwa nguvu na kumwangalia tena mwanamke huyo…

“Baby,” aliita Magembe.

“Nani baby wako? Yaani unataka kuniua kwa Ukimwi halafu unaniita baby! Mimi siyo baby wako kuanzia leo,” alisema mama Monica na kusimama, akaondoka huku akiendelea kulia lakini kiaina ili watu wasijue.

Alipofika nyumbani, aliingia chumbani kulala na mume wake aliporejea, alimkuta kitandani…

“Wewe una nini mpaka umelala muda huu?”

“Kichwa kinanigonga sana baba Monica, toka mchana mpaka nimelia.”

***

Wiki moja mama Monica hakutoka ndani. Alikuwa akiwapa maagizo wasichana wake wa kazi. Muda mwingi alikuwa akilia, aliamini Magembe alifanya makusudi kumshawishi atembee naye ili amwambukize Virusi vya Ukimwi…

“Kama kweli angekuwa hana angenitafuta. Wiki nzima sasa, lazima atakuwanao. Baba muuaji sana yule,” alisema moyoni mama Monica na kumwaga machozi, kisha akajikuta akishika simu, akamtumia meseji Magembe…

“Mzima wewe?”

Zilikatika dakika kumi, ndipo meseji yake ikajibiwa…

“Mi mzima, nilikuwa hospitali ndiyo maana nimechelewa kujibu meseji yako.”

“Hospitali unaumwa au?”

“Kupima Ukimwi.”

“Mh!” aliguna mama Monica…

“Huamini au?”

“Siamini. Kwa nini uende peke yako?”

“We si ulitoka kwa hasira siku zile.”

“Hata ungekuwa wewe ungetoka kwa hasira. Haya, majibu yakoje?”

“Mimi nilishakwambia niko fiti, karatasi langu la majibu ninalo hapa.”

“Wao…kweli baby?”

“Kabisa. Hapa natafuta mahali nikakae nipate bia hata tatu, roho yangu ina amani sana.”

Mama Monica alipata nguvu ghafla, akatoka kitandani, akasimama…

“Unakwenda kupatia wapi bia? Nije uninunulie na mimi?”

“Njoo. Nakwenda palepale Tip Top.”

Mama Monica alijimwagia maji, akajipodoa, akatoka bomba sana. Siku hiyo alitinga suruali ya jinsi na t-shirt.

Wakati anatoka akamtumia meseji mumewe…

“Baba Monica kidogo leo nimejisikia vizuri ngoja niende nikawaangalie wasichana wangu na biashara pia.”

Alitembea mpaka kwenye usafiri wa Bajaj, akachukua mpaka Tip Top ambapo alimkuta Magembe amejaa tele ndani ya baa…

“Vipi baby?” ndiyo ilikuwa salamu ya mama Monica huku akimwinamia na kumbusu Magembe…

“Mmm…mwaaa…”

Magembe aliachia tabasamu, akakumbuka mara ya mwisho kukaa hapo na mwanamke huyo na jinsi alivyoondoka akilia, leo hii anaingia na mabusu motomoto…

“Karibu sana baby.”

“Asante, za kwako? Za nyumbani kwenu? Za kunisusa?”

“Mimi nipo tu,” aliitika Magembe.

Mhudumu alifika, akatakiwa kumsikiliza mteja mgeni. Mama Monica aliagizia bia ya bariiidi!

Waliongea huku wakinywa, mpaka ikagota saa mbili usiku. Mama Monica wazo kwamba giza limeingia hakuwa nalo…

“Sasa?” aliuliza Magembe…

“Nini tena baby wangu?”

“Twende gesti basi.”

“Ha! Bwana! Muda kama umekwenda, hivi saa ngapi kwanza saa hizi?” alisema mama Monica na kuchukua simu ili aangalie saa…

“Mungu wangu, saa mbili unajua!”

“Kwani wewe mtoto,” alisema Magembe huku akisimama. Alilipa wakatoka kwenda gesti ya jirani. Walichukua chumba, wakaingia uwanjani…

“Nikwambie kitu baby?” alisema mama Monica huku akicheza kabumbu…

“Niambie mpenzi wangu.”

“Yaani leo nina furaha, hata kama nitakwenda kugombezwa na mume wangu niko tayari. Maana lo! Lakini cheti ulichopimia Ukimwi si umesema unacho?”

“Wewe…mimi nilikuwa nakudanganya, sijapima Ukimwi wala virusi.”

 

Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi, Jumatano ijayo.

 

 

Leave A Reply