The House of Favourite Newspapers

WASAFI FESTIVAL: KILICHOMKUTA DIAMOND SUMBAWANGA, HATOSAHAU

NI hekaheka! Mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amekiona cha moto baada ya kundi la vijana kumvamia, kumzonga kwa saa kadhaa wakidaiwa kutaka kumpora, Ijumaa Wikienda lilikuwepo.

NI IJUMAA ILIYOPITA

Tukio hilo lilijiri Ijumaa iliyopita baada ya jamaa hao kumvamia, mara baada ya kuwasili wilayani Sumbawanga kwa ajili ya kufanya tamasha maarufu kwa jina la Wasafi Festival.

WAHUNI SIYO WATU WAZURI

Vijana hao waliosemekana ni wahuni maarufu wilayani Sumbawanga, walionekana kudhamiria kwani walitega ‘mingo’ yao jirani na Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga na Diamond aliposhuka tu, wakamvaa. “Hawa jamaa unaowaona ni vibaka maarufu sasa pale kama unavyoona wanataka kumkomba kila kitu, wanajifanya kama mashabiki kumbe wana lao jambo, angalia wanavyomzonga na kuingiza mikono yao katika koti la Diamond,” alisikika sahabiki mmoja wa Diamond aliyejitambulisha kwa jina la Konki.

MABAUNSA WAPATA WAKATI MGUMU

Hekaheka za vijana hao kutaka kupora zilionekana kuwapa wakati mgumu mabaunsa wa Diamond hadi pale wanausalama walipofika kuwasaidia, lakini hata hivyo, baadhi ya vijana hao walishafanikiwa mikono yao kufika kwenye mwili wa Diamond.

WAAMBULIA PATUPU

Hata hivyo, licha ya vijana hao kumzonga Diamond kiasi cha kumfanya akose pumzi kwa takriban dakika 30, hawakuweza kufanikiwa kumpora mkali huyo wa Wimbo wa Far Away zaidi ya kumvuta koti lake bila mafanikio.

MMOJA ATOLEWA MFANO

Baada ya ulinzi kuongezeka, kuna wakati jamaa mmoja aliyedaiwa kuwa miongoni mwa wale vibaka (aliyevuliwa shati pichani ukurasa wa mbele) alidandia gari la matangazo ambalo Diamond na wasanii wake walikuwa kwa juu wakilinadi tamasha lao akitaka kumvua viatu ndipo maafande walipomshtukia na kuanza kumvurumishia virungu vya kufa mtu na kumuonya.

AMEWEKA REKODI

Mashabiki wa burudani mjini hapa waliozungumza na paparazi wetu walisema katika miaka ya hivi karibuni hakuna msanii yeyote wa muziki aliyewahi kupata mapokezi kama hayo, wengi hawakuwa wakiamini kama kweli msanii huyo angefika kweli wilayani Sumbawanga. “Hii ni rekodi ameweka Diamond, hatujawahi kumpokea msanii kwa mapokezi makubwa kama haya, hatukutegemea kwa kweli,” alisema Haji Seif, mkazi wa Sumbawanga.

MADAKTARI, WAGONJWA…

Katika hali isiyokuwa ya kawaida madaktari na wagonjwa wa Zahanati ya Mzavas iliyopo mjini hapa walilazimika kutoka wodini kukimbilia nje kumuona Diamond aliyekuwa akipita na msafara eneo hilo. Diamond na kruu yake walipokuwa wakipita barabarani nje ya hospitali hiyo, wafanyakazi kadhaa wenye makoti meupe na vipima-joto walionekana kuwa ni madaktari walitoka wodini na kwenda kumlaki Diamond.

WAZAZI NAO WAMO…

Si madaktari tu, kuna wazazi waliowapeleka watoto kwenye hospitali hiyo na wagonjwa kadhaa nao walionekana kutoka wodini kwa ajili ya kumshangilia Diamond aliyekuwa kwenye gari la wazi na kundi lake la Wasafi Classic Baby (WCB).

DIAMOND KAMA PREZIDAA

Diamond alipowaona madaktari na wagonjwa aliwapungia mikono kama vile afanyavyo Rais au viongozi mbalimbali wa Serikali wanapolakiwa na wananchi ambapo nao walimpungia mikono kwa furaha.

HOTELINI SASA…

Mashabiki wa burudani walivamia Hoteli ya Kalabo Falls wakitaka kumuona Diamond hali ambayo ilisababisha mabaunsa wa Diamond kupata wakati mgumu kuwatawanya. Licha ya Diamond kufanikiwa kuingia hotelini, mashabiki hao hawakukubali kushindwa, wakaamua kupanda kwenye ukuta wa geti hilo na kuibukia ndani kulazimisha kumuona Diamond ambaye wakati huo alishajifungia chumbani.

MABAUNSA WAOMBA MSAADA

Baada ya kuonekana hali hiyo inaweza kuhatarisha amani kwani mabaunsa walishazidiwa nguvu, ikabidi waombe msaada wanausalama wilayani hapa ndipo ilipofika gari jingine la Polisi aina ya Land Cruiser XL maarufu kama Difenda. Baada ya Polisi wenye silaha kufika, kwa kushirikiana na mabaunsa wa Diamond walifanikiwa kuwatawanya mashabiki hao waliokuwa wakitaka kuendelea kumuona Diamond.

POLISI WAKITA KAMBI

Hata hivyo, Polisi walilazimika kumwekea ulinzi maalum usiku kucha hotelini hapo kwa ajili ya kufanya maangamizi ya Wasafi Festival yaliyofanyika usiku wa kuamkia jana kwenye Uwanja wa Nelson Mandela.

Comments are closed.