The House of Favourite Newspapers

Wasanii Bongo Acheni Kukopi, Kupesti

0

WAKATI wa tuzo za B.E.T sala na dua zilifanyika kumuombea Diamond ashinde tuzo aliyokuwa akiishindani na wasanii kutoka Nigeria, Burna Boy na Wizkid.

 

Wapo waliobeza uwezo wa wasanii huyo wa Bongo kupaa kimataifa na kushinda tuzo, lakini mimi na wenzangu kwenye kipindi cha Hot Pot tulisema: “Moja shika inazidi kumi nenda.”

 

 

Hakika tulijivunia siyo kushinda bali hata Diamond kuchaguliwa kuwania tuzo hizo, tulisema “muziki wetu unakua.”

 

 

Muziki wa Bongo umetoka kuwa uhuni enzi za miaka ya 90 na mwanzoni mwa 2000 hadi kuwa biashara hakika ni jambo la kuwapongeza wasanii wetu.

 

Pamoja na pongezi hizo kuna jambo la kutafakari “HIVI VIONJO VYA MUZIKI WA BONGO FLEVA NI VIPI?”

 

Baadhi ya watu wanasema, Bongo Fleva imetokana na vionjo vya muziki wa Hop Hop wenye asili ya Marekani ambao enzi hizo wasanii wa Kibongo walikuwa wanaiga Beat na kuziimba kwa Kiswahili.

 

Mageuzi mengi yamefanyika tangu mwaka 1996 ambapo jina rasmi na Bongo Fleva yaani “muziki wa kizazi kipya” lilipoanza kutumika na kukubaliwa rasmi.

 

Pamoja na hayo sitaki kueleza historia lakini ni wazi wasanii wetu wanatakiwa kujiuliza je, bado wako kwenye staili ya kuiga beat za wasanii wa nje na kuziimba kwa Kiswahili kama walivyofanya akina Mac Muga?

 

Kinachosikitisha hivi sasa ni kuona kuna baadhi ya wasanii tena wakubwa bado wanaendekeza mambo ya kukopi na kupesti sanaa za wasanii wa nje halafu kubaki na fikra kwamba baadaye watakwenda kushindana nao kwenye tuzo.

 

Wakati Mac Muga akikopi beat za Wamarekani hakutaka kwenda kushindana nao bali alikuwa anatoboa njia ya muziki wa kizazi kipya uweze kujulikana.

 

Hivi sasa muziki umeshajulikana, vipi wasanii wetu wanaendelea kuwa wazee wa kukopi na kupesti?

 

Wasanii wa Bongo wamekopi sana staili za Kinaijeria, wamekopi mno staili za Wamarekani na sasa wanaendelea kukopi staili za Kisauzi na Kikongomani.

 

Juzikati Diamond alishirikishwa na msanii Innoss B kwenye wimbo wake wa Yope ukiwa kwenye mahadhi ya Kikongo na kufanikiwa kushika chati YouTube.

 

Baadaye msanii huyo alinogewa akamwita Koffi Olomide na kufanya naye ngoma aliyoiita Waah; masebene kama yote.

 

Utamu ulipozidi msanii Nandy naye akamvuta Koffi, Harmonize yeye aligeuza upepo na kwenda kwa Awilo lakini staili ya kucheza na kuimba ni ileile ya Kikongo.

 

Kabla mate hayajakauka, Wasauzi walikuja na staili yao ya

Amapiano tayari wazee wa kukopi na kupesti wameamka, kila msanii anataka kufanya staili hiyo.

 

Jambo hili siyo baya lakini linapokuwa desturi linaundolea heshima muziki wa Bongo Fleva kimataifa.

 

Kwani Singeli ikiendelezwa haiwezi kutusua jamani, mbona Zuchu, Hamisa Mobetto na Prof Jay wameimba Singeli na imeshika chati?

Huyu Rais wa Kitaa anayetamba mitandaoni kwa sasa namaanisha Nay wa Mitego kaimba kikongo? Jibu ni hapana!

 

Kwa mantki hiyo tunaweza kukopi lakini tusinogewe hadi kupitiliza; wenzetu Wanigeria na Wasauz hawakopi Bongo Fleva yetu kiasi cha kujisahau. Ni hayo!

Na Rich Richard

Leave A Reply