The House of Favourite Newspapers

Wasanii: Tamasha la Serengeti Festival Limefungua Njia 2021

0

TAMASHA la kwanza la Muziki na Sanaa nyingine, la Serengeti (Serengeti Music Festival) jana lilianza kwa kishindo kikubwa katika jiji la maraha la Dar es Salaam.

 

Likipambwa na baraka ya mvua kubwa iliyonyesha jana mchana Dar es Salaam na baadaye usiku, wasanii wa Tanzania wamepata kile walichokitafuta sana “platform ya pamoja na ya kitaifa na kikataifa zaidi,” anasema Inspekta Haroun msanii mkongwe.

 

Likichanganya urithi wa Tanzania katika sanaa mbalimbali kuanzia uga wa sanaa za ngoma za asili, sarakasi na kisha jioni wakali wa Bongo fleva kuonesha uwezo wao, Tamasha hilo lenye malengo ya kuunganisha utalii na sanaa, limeanza na limeweka viwango.

“Hapa nipo jukwaa la watu mashuhuri, angalia mwenyewe nilipo najihisi niko katikati ya Hifadhi ya Serengeti, kuna picha za wanyama kama Simba, Tembo na Swala na uoto wa asili wa majani kama mbugani, hivi ni viwango vikubwa vimewekwa,” alisema mwakilishi wa kampuni ya Simu ya TTCL, mmoja wa wadhamini wa Tamasha hilo.

Kivutio kikubwa alikuwa mkongwe DJ Boniface Kilosa (aka Bon Love), DJ na mtayarishaji mkongwe na manju kuwahi kutokea katika nchi hii ambaye jana, kwa utamu wa Tamasha lenyewe, alirejea kwenye mashine ya one-on-two kuwachezesha wasanii wa zamani.

 

Hapo ndipo mamia ya mashabiki waliojitokeza Uwanja wa Uhuru na maelefu zaidi waliofuatilia live kwenye tv na mitandaoni, waliposhangazwa kusikia muziki mzuri kutoka kwa wasanii walioonekana wameshapotea katika anga la muziki kama Wagosi wa Kaya, Z Anto, MB Dogg na wengine.

“Dah ilikuwa bonge la memorylane, nahisi kutokwa machozi,” alisema shabiki wa muziki mara baada ya kumsikiliza Z Anto ambaye jana aliwasarprise mashabiki zake alipopanda stejini na Sandra, mkewe wa zamani na mwanadada aliyepata kuigiza kama kiziwi enzi za hit song ya “Binti Kiziwi.”

 

Ulikuwa usiku wa “back to back” hasa katika historia ya muziki, bado mashabiki walipata show kali kutoka kwa wakali kama Baby Madaha, Wylumva Mmarekani mwenye asili ya Tanzania kutoka New York, TID, THT, Gozbert Goodluck, Chid Benz na Weusi.

“Tumeweka viwango, tumewapa vijana platform na tumeanza, hatujamaliza,” alisema Rodney Thadeus kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, waratibu wa Tamasha hilo.

 

Tamasha la Serengeti linaendelea leo mjini Bagamoyo, Pwani, ambako litaungana na Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni kuanzia saa 12 jioni ambapo pamoja na ngoma na sanaa zingine pia wakali kadhaa wa muziki wa kizazi kipya kutoka Dar es Salaam na kwingineko wataperform.

Leave A Reply