The House of Favourite Newspapers

Wasanii wabwia unga wanaponzwa na ujuaji

q-chief-42-of-248Makala: Ojuku Abraham | Gazeti la Risasi Jumatano, Toleo la Jan. 11, 2017

NIMEISHI na wajuaji na nimewaona wanavyofeli. Kile kitendo tu cha kujiona unajua, tayari ni tatizo la msingi katika maisha ya kila siku ya binadamu, hasa vijana.

Rudi nyuma hata wakati ukisoma au kama upo shule kwa sasa, waliokuwa watiifu kwa walimu na sheria za shule, huku wakikazana kusoma, walionekana washamba, wakuja. Walikebehiwa na kudhihakiwa na wakati mwingine hata kufanyiwa vitendo vya kidhalilishaji. Leo hii ndiyo ma-CEO!

young-dee1Young D

Nina bahati sekondari niliyosoma, haikuwahi kumtoa mbabe wa kunionea, wote walikuwa marafiki tangu kidato cha kwanza, ingawa washkaji zangu wengi walilia kuonewa. Baadaye, wale wababe walifeli masomo, kwa sababu hawakuwa na muda wa kusoma.

Walipoingia mtaani, waliangukia kucheza mpira ambako pia walikuwa wavuta bangi. Baadhi yao walifanikiwa sana uwanjani, lakini wakakosa nidhamu ya maisha na leo tunapozungumza, wengi wao wameishia kubwia unga au wamezidisha kilevi na kupoteza mwelekeo.

Hata huku mitaani pia, kuna ujuaji. Mimi ni wa kuja, kwetu mkoa huko. Nilipoingia mjini miaka mingi iliyopita, tuliwakuta watoto wa mjini. Wakati tukipiga debe kwenye mitumba pale juani mtaa wa Kongo, watoto wa wenyeji Kariakoo walikuwa wakituona washamba, wakishinda uani kwao kivulini wakivuta bangi, wakitegemea wazazi wao kupata hela kwa kulipwa pango kwa wanaoweka meza mbele ya nyumba zao, au wakitegemea kulipwa kwa kuhifadhi mizigo usiku.

Chid-Beenz_fullChid Benz

Na wajuaji wale wa Kariakoo, usiku, walikuwa wakiipekua mizigo iliyohifadhiwa kwenye nyumba zao, wakiiba vitu, kesho yake wanang’aa kwa pamba safi, viatu na vingine wakiuza ili wapate hela ya kutanulia. Hawakuwahi kupiga debe au kuuza mitumba wajanja wale. Maisha yakaenda hivyo, vijana kutoka mikoani wakawa wanakuja baada ya muda wanafanikiwa, huku wale vijana wa mjini, wakihama kutoka kwenye bangi na kuingia kwenye ubwiaji unga!

nandoNando.

Nimezunguka kidogo hapa mjini na nimegundua kitu kimoja, wala unga wote ni watoto wa mjini, wajuaji. Watu wanaojitambua, wanaojua nini wanataka katika maisha yao, wakikutana na wajuaji hawa, wanaonekana washamba.

Kizazi cha kwanza cha Bongo Fleva, kilikuwa kizazi cha waliojitambua, waliojua nini wanataka, ndiyo maana hata kama nyota zao zimefifia hivi sasa, lakini si ombaomba, wana maisha nje ya muziki. Kama unga, angekula Sugu, ambaye wauza unga wote walitamani awe rafiki yao.

MangweaNgwea.

Profesa Jay angeweza kuwa teja mzuri, kwa sababu angeupata kwa kutumia jina lake tu. Hata Juma Nature, wakati ule ameikamata Bongo Fleva angeweza ‘kusniff’, lakini alijitambua. Mastaa wa enzi hizo ni wengi mno, Inspekta, Soggy, Dudubaya, Mike T na wenzao walijitambua.

Siyo kwamba hakukuwa na wasanii wenye kula vilevi. Walikuwepo, lakini wengi walifuata ushauri wa Jay Moe, walikula ‘mmea’ kwa sababu poda noma!

Kizazi hiki cha Bongo Fleva, kimejaa wajuaji. Kuna wanaodhani kusafiri nje ya nchi ni wao ndiyo wameanza, wakisahau kuwa kaka na dada zao walianza kufanya hivyo kabla wao hawajazaliwa au wakiwa ‘vidudu’. Waangalie wala unga katika muziki wa kizazi kipya hivi sasa, baadhi yao ni vijana flani ambao mwaka 2000, wote walikuwa watoto, wakijazana pale Coco Beach kila wikiendi wakati Juma Nature akiwarusha.

natureNature

Wenzao walichagua ‘mmea’ kwa sababu unaachika. Terry Fanani alipotezwa na unga na hadi leo analia, anapigana kuacha na Mungu amsaidie. Afadhali Q-Chillah alikiri udhaifu, akampigia magoti Mungu wake na sasa maisha yamerejea.

Lakini kuna wasanii ambao ndiyo kwanza wameanza kuvaa suruali katikati ya makalio, wanaona ujanja kubwia unga na ukiwauliza, wanakuja juu hatari. Hivi sasa kuna orodha ndefu ya wasanii wanaokula ‘poda’, wengine wamejidhihirisha, wengine wanaonyesha dalili na wapo ambao wanajitutumua kukomaa wasijulikane. Hawajui kuwa huwezi kujificha kuhusu ulaji unga, tena huu wa daraja la chini kama wanaotumia wao. Ni kama mnazi, ukiupanda uani, utakua na kuipita nyumba.

langa-1Langa

Sisi washamba kutoka mkoa, tunaamini kabisa ni ulimbukeni wa hali ya juu kijana kula unga. Kaka na wadogo zetu wengi wa pale Magomeni, Mwananyamala, Ilala na Kinondoni, sehemu ambazo unga umeanza kuuzwa enzi na enzi, mwisho wao ulikuwa ni kufa kwa fadhaa.

Unga umewaua wasanii wakubwa Marekani na Ulaya, tena wenye mamilioni ya dola na kwenye hospitali zenye uwezo wa hali ya juu kimatibabu, sembuse Bitozi Nyangema, hela yako ya ngama hata msingi wa maisha yako hujaweka na hospitali hizi ambazo hata panado ni ishu?

Take Care!

Comments are closed.