The House of Favourite Newspapers

Lwandamina Ataka Yondani Awe Mshambuliaji

YONDANI

Beki wa Yanga kisiki, Kelvin Yondani.

Omary Mdose na Said Ally

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina, amezidi kuwashangaza wengi baada ya kutamka kuwa siku za usoni anatarajia kuwaona mabeki wake wakicheza nafasi za ushambuliaji.

Kauli ya Lwandamina imekuja siku chache baada ya kuanza kubadilisha mfumo wa uchezaji ndani ya kikosi hicho huku akiwabadilishia majukumu ya uwanjani wachezaji wake akiwemo Juma Mahadhi, Oscar Joshua na Geofrey Mwashiuya.

Mahadhi ambaye ni winga, siku za karibuni amekuwa akichezeshwa kama straika, huku Joshua anayemudu beki ya kushoto, juzikati alichezeshwa nafasi ya straika, wakati Mwashiuya ambaye ni winga, akichezeshwa beki wa kushoto.

Watu wengi wamekuwa wakishangazwa na hali hiyo ambayo imeanza kujitokeza kikosini hapo tangu Mzambia huyo akabidhiwe kikosi hicho, Novemba, mwaka jana.

Akizungumzia hilo, Lwandamina amesema: “Katika soka la kisasa, mchezaji anaweza kucheza nafasi yoyote uwanjani, lengo likiwa ni kusaidia sehemu ambayo inaonekana kuwa na mapungufu ili kufanikisha kile mnachokitaka.

“Katika mfumo huu usishangae kuona mchezaji akicheza nafasi ambayo hajaizoea, anaweza kucheza kama mshambuliaji, kiungo au hata beki, hili linaweza kutokea kwa wote lakini mchezaji pekee ambaye hatahama nafasi yake ni kipa tu kutokana na sheria kutoruhusu,” alisema Lwandamina.

Kwa mantiki hiyo, mfumo huo wa Lwandamina unaweza kumlazimu beki wake kisiki, Kelvin Yondani kuchukua mikoba ya Amissi Tambwe au Donald Ngoma kwenye ushambuliaji kama ikitokea siku mastraika hao hawapo.

 

Comments are closed.