The House of Favourite Newspapers

Washtakiwa 5 Uhujumu Uchumi Wakiri Makosa

WASHTAKIWA watano wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi akiwemo wakili, Dk Ringo Tenga, wamemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuomba kukiri makosa yao. Wakili wa washtakiwa hao, Bryceson Shayo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana Ijumaa Septemba 27, 2019 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

 

Dk Tenga ambaye ni Mkurugenzi na Mwanasheria wa Kampuni ya Mawasiliano ya Six Telecoms Limited na wenzake, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 73/2019. Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.

 

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha, na Kampuni ya Six Telecoms.

 

Wakili Shayo amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kuwa wamejadiliana na wateja wao na baada ya majadiliano hayo wameamua kumuandikia DPP barua kwa kuzingatia maagizo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa Septemba 22, 2019.

 

Amesema kutokana na uamuzi huo, wanaiomba mahakama kutoa ahirisho la siku 14 kuanzia leo ili waweze kupata majibu ya barua hiyo. Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 11, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Comments are closed.