The House of Favourite Newspapers

Kiki za Mapenzi Ziliwapaisha

KATIKA ulimwengu wa mastaa kuna mambo mengi sana yanayoendelea yakiwemo mazuri na mabaya ambapo wasanii wamekuwa wakifanya kiki za aina mbalimbali ili tu waendelee kuwa juu.

Wapo mastaa ambao walikuwa chini na hawakuwa wanasikika tena kwenye ulimwengu wa sanaa au walikuwa wanasikika ila siyo kivile lakini walipobuni mbinu za kurudi kwa upya waka-amua kutoka na kiki za mapenzi.

 

Mastaa wengi wanaamini kuwa mapenzi yanalipa ndiyo maana kila anapotaka kurudi kwenye gemu baada ya kutosikika kwa muda mrefu anakuja na kiki ya mapenzi lakini mwisho wa siku inakuja kugundulika kuwa haikuwa kweli ilikuwa ni kiki kwa ajili ya kazi mpya.

Katika makala haya tunakuletea baadhi ya mastaa ambao walitoka na kiki za mapenzi na zikawapaisha kwa wakati husika huku watu wakiamini kuwa ni kweli kumbe ni njia ya kuwateka ili wawafuatilie kazi zao.

 

MLELA NA EBITOKE

Yusuph Mlela na Anna Exavery ‘Ebitoke’ ni waigizaji wa filamu za Kibongo. Wawili hawa hivi karibuni walikuwa ni gumzo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kutokana na mahaba yao ambayo walikuwa wakiyaonesha hadharani.

Awali wawili hawa kila walipokuwa wakiulizwa kuhusiana na uhusiano walikuwa wakikiri kuwa ni wapenzi lakini ukweli umejulikana hivi karibuni kwamba walikuwa wakitengeneza filamu mpya ya mahaba inayojulikana kwa jina la Mahabamarhaba hivyo walifanya hivyo kuwaweka mashabiki zao karibu.

 

NANDY NA BILNASS

Licha ya wanamuziki hawa Faustina Charles ‘Nandy’ na William Lyimo ‘Bilnass’ kuwahi kuwa wapenzi na kuachana, siku za hivi karibuni wameibuka tena na kuzua gumzo kila kona.

Wawili hawa walikuwa wakioneshana mahaba kila kona na walipoulizwa walisema wamerudiana lakini wadadisi wa mambo waligundua kwamba ilikuwa ni kiki kwa ajili ya ngoma yao mpya ya Bugana.

 

SNURA NA MINU

Japokuwa baadaye walikuja kuwa wapenzi kweli, wasanii hawa wa muziki Snura Mushi na Minu Calypto mwanzoni walianza kwa kiki kuwa ni wapenzi ili kuwa juu kwenye sanaa yao.

Penzi lao la kiki lilikuwa ni gumzo kubwa am-bapo baada ya kuwa penzi kweli hawakudumu kwa muda mrefu, wakamwagana.

 

SISTER FAY NA HOLY STAR

Faidha Omary ‘Sister Fay’ ni msanii wa filamu na muziki ambapo awali alianza kama kiki kwa kusema kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na msanii chipukizi wa muziki, Holy Star.

Penzi lao la kiki likaja kuwa kweli ambapo watu hawakuamini kwani Holy Star kiumri ni mdogo sana kwa Sister Fay na baada ya hapo waliingia kwenye ndoa, yaani wakafunga ndoa ya Kiislamu.

Ndoa ya wawili hawa ilidumu kwa muda mfupi na kuvunjika ambapo kwa sasa kila mtu ana maisha yake.

 

SHAMSA NA NAY WA MITEGO

MSANII wa filamu Shamsa Ford na mwanamuziki Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ penzi lao lilitikisa sana kwa kipindi hicho ambacho Nay alikuwa akitikisa.

Penzi hilo lilivunjika na kila mmoja kuendelea na maisha yake ambapo Shamsa aliolewa lakini ndoa yake imevunjika hivi karibuni huku Nay akiwa hajaingia kwenye ndoa bado.

GLADNESS MALLYA

Comments are closed.