The House of Favourite Newspapers

Wasidi: ‘Waafrika waliopotelea’ India!

0

SI Wahindi weusi!  La Hasha!  Wanaishi India na inasemekana mababu zao walianza kuishi sehemu hiyo ya dunia tangu karne ya 12.  Kwa Kiingereza wanajulikana kama Sidis.

Wanaitwa “Waafrika waliopotelea” wa India.  Kwa kifupi, ni Waafrika kabisa!  Ni weusi, wana nywele za kipilipili na kadhalika.  Ni Waafrika kama walivyo Waafrika wa Nigeria, Kenya, Tanzania na kwingineko.  Ukikutana nao maeneo ya Mwanza utajua ni Wasukuma halisi!

Kutokana na jamii za India zilivyo, watu weusi hao siku zote wameishi maisha ya kutengwa kutokana na rangi yao wakiwa miongoni mwa “watu wasioguswa”!  Wataalam wa historia wanasema watu hao ni mabaki ya watumwa ambao mababu zao walichukuliwa, hususani na Wareno, na wafanyabiashara wengine na kupelekwa India ambako baada ya utumwa kupigwa marufuku waliendelea kuishi huko na idadi yao kuongezeka polepole kwa miaka ikaribiayo 1,000 sasa.

Wengi wa watu hao walikamatwa kutoka Afrika Mashariki kwenye kuajiriwa kama askari, waburudishaji na watumwa katika mashamba nchini India.

‘Waafrika’ hao hivi sasa wengi wao wanaishi katika majimbo ya Gujarat na Karnataka kusini mwa nchi hiyo.  Kwa Waafrika ambao  wamewahi kufika India, watakuwa wamewaona watu hao pia katika sehemu zingine za nchi hiyo.

Wasidi, ambao idadi yao inaishia kwenye makumi ya maelfu na wengi wakiwa maskini, wameendeleza utamaduni wao wa Afrika katika fani mbalimbali hususan kutokana na kutengwa na jamii ya Kihindi.

Wengi wao ni Waislam na Wakristo, kwani kutokana na jamii inavyowachukulia, si rahisi kwao kujiunga na dini zingine za watu wa asili ya nchi hiyo.  Kuna mabaki pia ya Wasidi kusini mwa India, Sri Lanka, Goa, Iran na Afghanistan.

Leave A Reply