The House of Favourite Newspapers

Watatu wafariki, 5 hospitalini baada ya kunywa mkorogo

WATU watatu wameripotiwa kufariki na wengine watano wakilazwa hospitalini baada ya kunywa dawa ya miti shamba katika kijiji cha Tabani, eneo bunge la Tongaren kaunti ya Bungoma, Kenya. 

Inasemakana kuwa wanane hao walikunywa dawa hiyo waliyopokea kutoka kwa daktari wa miti shamba ambaye alidai ilikuwa na uwezo wa kuponya maradhi mbalimbali.

Watu hao, akiwemo mwanamke na mamake mkwe, walifariki takriban dakika tatu baada ya kunywa dawa hiyo huku wengine wakikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Moi.   Mmoja kati yao ambaye alikuwa katika hali mbaya alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Judith Situma ambaye ni binti wa mmoja wa wanawake waliofariki, alifichua kwamba mamake ambaye alikuwa na maumivu kifuani alitafuta matibabu kutoka kwa daktari wa miti shamba.

“Ni masikitiko makubwa kumpoteza mama wakati alikuwa ndiye mzazi pekee niliyekuwa nimesalia naye. Sielewi kilichotokea kwa kuwa hii sio mara ya kwanza kwa mama kwenda kwa daktari huyo. Tumeshikwa na mshtuko mkubwa hatujui tuanzie wapi,” Situma alisema.

Wakazi wa eneo hilo wamewataka polisi kumkamata daktari huyo na kumchukulia hatua  za kisheria.

Chanzo: Tuko Newspaper 

Comments are closed.