The House of Favourite Newspapers

WATEKAJI KUNDI LA WEZI WA WATOTO LATAJWA

WIMBI la utekaji watoto linazidi kutikisa ambapo katika siku za hivi karibuni wameshatekwa watoto watatu huku wengi wakihoji ni nani hasa wanahusika na utekaji huo? Risasi Mchanganyiko limechimba na kuibuka na kundi ambalo liko nyuma na matukio hayo.

Mtoto Beauty Yohana (3) wa Kimara jijini Dar ndiye wa kwanza kuibua taharuki kubwa siku za hivi karibuni baada kutoweka katika mazingira ya kutatanisha alipokuwa kanisani ambapo alipopatikana ndani ya saa 48, zikaibuka taarifa nyingine za mtoto aliyefahamika kwa jina la Idrissa Ally ambaye naye anadaiwa kutekwa.

 

TUKIO LA KUTEKWA BEUTY

Huyu alidaiwa kutekwa akiwa kwenye Kanisa la FPCT lililopo Mbezi-Mwisho jijini Dar, lakini baadaye alipatikana maeneo ya Kivule akiwa na binti aitwaye Angel Vincent (19) aliyedai alidhamiria kumpeleka kwa bibi yake anayefanya mambo ya kishirikina.

 

SIMULIZI YA KUTEKWA KWA IDRISSA ALLY

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 13 alitekwa kimafia na mtu asiyejulikana akiwa anacheza na wenzake huko Tegeta-Masaiti jijini Dar. Inaelezwa kuwa, wakati akicheza lilitokea gari aina ya Toyota IST na dereva wa gari hilo alianza kuzungumza na mtoto huyo kabla ya kumchukua na kumpandisha katika gari huku akitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa ni ‘spray’ na kumpulizia usoni.

 

Akisimulia tukio hilo, mama wa mtoto huyo, Leila Kombe alisema Idrissa alirudi kutoka shuleni saa tisa alasiri kisha saa 10:30 jioni na kuaga kuwa anakwenda kucheza na wenzake. “Alitoka nyumbani na baiskeli kisha alikwenda moja kwa moja hadi nyumba ya tatu alipokutana na watoto wenzake,” alisema.

Mama Idrissa aliongeza kuwa, akiwa kwenye genge hilo lilitokea gari aina ya Toyota IST lenye rangi ya silver likaegeshwa karibu na genge hilo kabla ya kumchombeza mtoto na kumchukua kisha kutoweka naye. Mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni, mtoto huyo alikuwa hajapatikana.

 

MWINGINE TENA AIBWA

Wakati wazazi wa Idrissa wakilia wasijue aliko mtoto wao, mtoto mwingine aitwaye Gabriela Kilimba (3), anadaiwa kuibwa akiwa amelala chumbani, nyumbani kwao Ukonga-Mazizini jijini Dar.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, baba wa mtoto huyo, Kilimba Geofrey alisema mwanaye akiwa na mama yake, Adrat Mwangia nyumbani kwao, alimuacha mtoto ndani akiwa amelala chumbani na kumfungia kwa nje kisha kwenda hospitali ya jirani kuchoma sindano ambapo alichukua kama dakika tano kwenda na kurudi.

 

Alisema mama wa mtoto aliporudi na kufungua mlango akashangaa kuona mtoto hayupo wakati alimfungia kwa nje. “Mke wangu nilipomuuliza mazingira ya mwanangu kupotea, hivyo ndivyo alivyoniambia.

“Yaani tumemtafuta kila kona bila mafanikio, tumeshapeleka taarifa mpaka Polisi na kufungua taarifa ya kupotea mwanangu kwenye jalada lenye namba MAZ/RB/1349/2018 TAARIFA YA KUPOTEA MTOTO,” alisema mzazi huyo. Akizidi kusimulia kwa uchungu, mzazi huyo alisema anasikitika kuona tatizo hilo la watoto kutekwa linazidi kushika kasi huku akishindwa kujua ni nani wako nyuma ya matukio hayo.

 

“Yaani kila nikimfikiria mwanangu sijui la kufanya, wenzangu watoto wao wanapotea na kupatikana, lakini mwanangu mpaka hivi tunavyoongea bado sijamuona,” alisema mzazi huyo na kuongeza: “Naomba yeyote atakayepata taarifa za kuweza kupatikana mwanangu anijulishe kupitia namba 0714447962 au 0756036440.”

 

GENGE LA WATEKAJI LATAJWA

Wakati hali ya hofu ikizidi kutanda kwa wazazi kufuatia matukio hayo ya mfufulizo, baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti waliyataja makundi ya watu ambao wako nyuma ya wimbi la utekaji wa watoto.

WENYE SHIDA NA WATOTO

Mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Asha Hamis wa jijini Mbeya alisema kuwa, moja ya makundi ya wanaoiba watoto ni baadhi ya wanawake waliohangaika kwa muda mrefu kutafuta watoto bila mafanikio.

 

“Matukio ya wanawake kukutwa na watoto wasio wao yamekuwa mengi, kuna mmoja hapa Mbeya aliwahi kukamatwa na mtoto ambaye amemuiba hospitalini ili naye aitwe mama,” alisema mama huyo.

Wapo waliotaja kundi lingine kuwa ni lile linalojihusisha na masuala ya kishirikina, hasa baada ya binti Angel aliyenaswa na mtoto Beauty kudai alikuwa ametumwa na bibi yake anayefanya mambo ya kishirikina.

“Kuna uwezekano mkubwa watu wenye imani za kishirikina wanahusika na utekaji wa watoto, yule Angel (aliyenaswa na Beauty) alisema huko alikotaka kumpeleka kuna watoto wengine, sasa hapo unaona kwamba kundi hili la washirikina linahusika na utekaji huu unaoendelea,” alisema Johnson Kibuti wa Kivule jijini Dar.

 

KUNDI LA MAFIA

Wengine wanaotajwa kuhusika na utekaji huo ni ‘Mafia’ ambao wamekuwa na tabia ya kuchukua watoto ‘kimafia’ kisha baadaye wanapiga simu kwa wazazi wao kutaka wapewe pesa ili wawarejeshe.

KISASI CHA MAHAUSIGELI

Katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili pia umekutana na baadhi ya watu ambao waliwataja baadhi ya mahausigeli waliokorofishana na mabosi wao kuiba watoto wakiwa na lengo la kuwakomoa.

 

NENO LA VIONGOZI WA DINI

Kufuatia kutajwa kwa makundi hayo yanayodaiwa kuwa nyuma ya utekaji wa watoto, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya viongozi wa dini ambao walisema kuwa, kinachotakiwa ni kusali na kuomba ili Mungu awakinge watoto wetu.

“Tumrudieni Mungu wetu, tusali na tuombe sana awalinde watoto wetu na majanga haya,” alisema Nabii James Nyakia wa Kanisa la Jerusalem lililopo Kitunda jijini Dar.

 

JESHI LA POLISI LINASEMAJE?

Akizungumzia utekaji huo wa watoto, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Muliro alisema kwa kuwa taarifa zimesharipotiwa, Jeshi la Polisi litazifanyia kazi.

Naye Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, ACP Salum Hamduni aliwataka wananchi wanaokutana na matukio ya kupotelewa na watoto wao wafike mara moja kwenye vituo vya polisi ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.

KUTOKA RISASI

Gazeti hili linawatahadharisha wazazi kuwa makini sana na watoto wao katika kila sehemu wanayokuwa ili kuwakinga na kundi la watekaji.

Comments are closed.