The House of Favourite Newspapers

MGONJWA ABOMOLEWA NYUMBA KIMAFIA

KAZI ni kwako! Mkazi wa Kimara- Golani jijiji Dar, Esther Mpari ambaye ni mgonjwa wa presha amemlilia Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kubomolewa kibabe, usiku mnene na mabaunsa.

 

Kwa mujibu wa mama huyo, alifikwa na sekeseke hilo baada ya mumewe, Grayson Maduje almaarufu Juma kuiuza kinyemela nyumba waliyokuwa wakiishi kwa shilingi milioni kumi na laki saba (10,700,000) na kumuacha akiwa hana pa kwenda kufuatia mabaunsa wa aliyenunua kumtoa kinguvu na mume wake kumkimbia.

 

Akielezea sakata hilo, Esther alisema Septemba 26, mwaka huu, majira ya saa nane usiku, walifika mabaunsa kwenye nyumba yake na kuanza kubomoa, yeye akiwa ndani na watoto wake kwa madai kuwa walielekezwa kufanya hivyo na mtu aliyeinunua nyumba hiyo.

 

“Hao mabaunsa walifika majira ya saa nane usiku mimi na wanangu tulikuwa ndani tumelala kisha tukasikia vishindo vizito ndipo tukataka kujua ni nini kimetokea hivyo tukatoka na kukutana nao uso kwa uso wakiendelea kuibomoa nyumba yetu.

“Nilianza kupiga kelele kuita majirani waweze kutusaidia.“Hatimaye nguvu ziliniishia, nikaanguka na kupoteza fahamu ndipo nikapelekwa Hospitali ya Mwananyamala (Dar) mpaka hali yangu ilipokaa sawa ndiyo nikarudi nyumbani na kukuta nyumba yote imeshabomolewa,” alisema Esther.

 

Alisema baada ya kutoka hospitalini, kwa kuwa hakuwa na mahali pa kuishi, aliwaomba majirani wamjengee kibanda cha muda pembeni mwa nyumba hiyo iliyobomolewa wakati akiendelea kufuatilia haki yake.

 

Kutokana na kukosa sehemu ya kuishi kiusalama, imebidi watoto wake wawili akawaombee hifadhi Ustawi wa Jamii Manispaa ya Ubungo huku yeye na mwanaye mkubwa wakiendelea kujibanza kwenye kibanda hicho. Mama huyo ambaye kwa sasa hajiwezi kutokana na hali ya kuumwa amemuomba Waziri Lukuvi amsaidie kupata haki yake kwa kuwa nyumba hiyo imeuzwa bila yeye wala watoto wake kushirikishwa.

“Namuomba Lukuvi anisaidie maana huyo mteja hata kama aliletwa kuikagua nyumba, mimi sijui alikuja saa ngapi na kwa nini hakutaka kufanya uchunguzi na kuongea na tunaoishi kwenye nyumba moja na sijui aliinunua kwa utaratibu gani,” alilalama mama huyo.

 

Wanahabari wetu walifika kwenye ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Kimara-Golani ilipo nyumba hiyo na kukuta bendera ya Serikali ikipepea na milango ikiwa wazi, lakini ndani hakukuwa na mhusika yeyote. Alipotafutwa mumewe ili kupata undani wa sakata hilo, namba ya simu iliyotolewa na mkewe haikuwa hewani hadi gazeti hili linakwenda mitamboni.

Stori: Zaina Malogo na Richard Bukos, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.