Kinamama Waliojifungua Na Watoto Zao Wazawadiwa Bima Za Afya 600 Na Kampeni ya Sambaza Shangwe Gusa Maisha
Kampuni ya mtandao wa simu za mkononi ya Vodacom imefanya kitendo cha kuirudishia jamii sehemu ya inachokipata kwa kuwazawadia bima za afya 600 watoto waliozaliwa katika Hospitali za Rufaa za Mwananyamala, Amana na Temeke pamoja na mama zao.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Meneja Mauzo Kanda ya Dar es Salaam George Nyanda amesema;
“Kwanza napenda niwashukuru wote mliofika kwenye tukio hili ambalo msingi wake mkuu ni kutoa bima za afya kwa watoto waliozaliwa pamoja na mama zao.
“Vodacom kila mwaka tumekuwa na kampeni maalum ya kurejesha kwa jamii sehemu ya tunachokipata ambapo kampeni ya mwaka huu tumeipa jina la “Sambaza Shangwe, Gusa Maisha” tukiamini tunawajibika kabisa kama taasisi ya kibiashara kugusa maisha ya wateja wetu na hata wasio wateja wetu.
“Katika kampeni yetu ya mwaka huu Vodacom tunahakikisha wamama na watoto 200 kwa kila hospitali zinaguswa na kampeni hii.
“Hii ni kampeni ya nchi nzima ambapo inatarajia kugusa wahitaji 2000 na mpaka sasa tumeshafanya mikoa tofauti kama vile Mbeya, Zanzibar na leo hii tuko hapa Dar es Salaam ambapo tutakuwa katika Hospitali zetu kuu tatu za kikanda hapa Mwananyala, Amana na Temeke”. Alisema George.
Meneja huyo alimaliza kwa kusema kwa mwaka huu wao kwa kushirikiana na Kampuni ya Bima ya Assemble wameamua kuangalia suala la afya ya mama na mtoto katika kipindi cha kujifungua.
Kwa upande wao Waganga Wafawidhi kutoka Hospital ya Mwananyamala, Amana na Temeke kila mmoja aliishukuru Vodacom kwa kuja na kampeni hiyo iliyoangalia suala la afya ya mama na mtoto ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakikosa huduma stahiki kwa kukosa pesa ya matibabu lakini bima hizo zitawasaidia kupata matibabu kwa muda muafaka.