The House of Favourite Newspapers

Watoto Wenye Ulemavu Mbeya Wafungukia Changamoto Zinazowakabili

sehemu-ya-watoto-wa-shule-ya-msingi-mwenge-wakiwa-kwenye-semina-hiyoSehemu ya watoto wa Shule ya Msingi Mwenge wakiwa kwenye semina hiyo.

afisa-mipango-wa-mbeya-milinga-akizungumzia-changamoto-za-watoto-walemavuAfisa Mipango wa Mbeya, Milinga akizungumzia changamoto za watoto walemavu.

lucas-mhenga-kulia-akiwa-kwenye-semina-hiyo Mtoto Richard ambaye ana ulemavu wa miguu akieleza changamoto zake.mtoto-richard-ambaye-ana-ulemavu-wa-miguu-akieleza-changamoto-zakeMtoto Richard ambaye ana ulemavu wa miguu akieleza changamoto zake.

mtoto-tusijigwe-msokwa-akieleza-changamoto-za-watoto-walemavuMtoto Tusijigwe Msokwa akieleza changamoto za watoto walemavu.

 

naibu-mbeya-wa-jiji-la-mbeya-david-ngogo-akifafanua-jamboNaibu Mbeya wa Jiji la Mbeya, David Ngogo akifafanua jambo.

Watoto wenye ulemavu kutoka sehemu mbalimbali nchini wameendelea kupaza sauti zao kupitia mabaraza ya watoto wenye ulemavu ambapo safari hii watoto kutoka Jiji la Mbeya walipata fursa hiyo.

Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) kwa kushirikiana na Taasisi ya ERIKS Development waliandaa semina mkoani humo iliyowahusisha watoto hao, wazazi pamoja na viongozi mbalimbali kutoka serikalini.

Akizungumza kwenye semina hiyo, mmoja wa watoto wenye ulemavu wa ngozi aliyejitambulisha kwa jina la Tusijigwe Msokwa anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Nzondali alisema, anachoona yeye jamii imekuwa na mtizamo hasi juu yao hivyo ni vyema watu wakabadilika na kuwaona wao ni kama watoto wengine.

 “Sehemu kubwa ya jamii ina mtizamo hasi kuhusu sisi kitu ambacho kinatukosesha amani mara nyingi, tunaiomba jamii ibadilike na kutuona sisi ni kama watoto wengine tunaostahili kupata kila wanachopata watoto wasio na ulemavu,” alisema mtoto huyo.

Naye Richard Musa Edward ambaye ana ulemavu wa miguu anayesoma kwenye Shule ya Msingi Mwenge alizungumzia juu ya mahitaji muhimu ambayo wanatakiwa kupatiwa ili kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo.

“Mimi kama mtoto mwenye ulemavu wa miguu, nahitaji baiskeli inayoweza kunisaidia lakini pia tunahitaji mazingira rafiki shuleni na kila sehemu kwani sehemu nyingi ni kama vile tumetengwa,” alisema mtoto huyo.

 Watoto hao wameeleza kuwa, wao wanao uwezo wa kufanya mambo makubwa katika jamii ila wanachotaka ni kujengewa mazingira rafiki ambayo yanaweza kuwawezesha kutimiza ndoto zao.

 Wakizungumzia changamoto hizo, baadhi ya viongozi kutoka Halmashauri za Jiji la Mbeya walionesha kuwa tayari kuwasaidia kwa kueleza kuwa, watajitahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo ili kutokuwepo kwa tofauti kati ya watoto hao na wale wasio na ulemavu.

“Kimsingi watoto hawa wana haki ya kupatiwa huduma zote za msingi na hilo ni jukumu letu hivyo tutakuwa pamoja nao na pale ambapo tunaona tunaweza kuwasaidia, tutafanya hivyo,” alisema Hope Kavuli ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Rungwe.

Naye Naibu Meya wa Jiji la Mbeya, David Nelson Ngogo kwanza aliwapongeza FPCT kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaleta pamoja watoto wenye ulemavu na kupaza sauti zao ili jamii iweze kuwasaidia.

 “Kwa kweli niwapongeze sana FPCT, wanafanya kazi kubwa ambayo inatakiwa kuungwa mkono, watoto hawa wakiachwa peke yao watakuwa wanaishi kwenye mazingira magumu hivyo ni vyema tukajitoa katika kuwasaidia,” alisema Ngogo na kuongeza:

“Lakini pia niseme tu kwamba mimi kama sehemu ya serikali tutahakikisha bajeti inatengwa ili iweze kuwasaidia watoto hawa katika mahitaji yao ya msingi majumbani na mashuleni pia.”

Akizungumza katika mjumuiko huo, mgeni rasmi ambaye ni Afisa Mipango wa Mkoa wa Mbeya, Conald Milinga kwanza alipongeza uanzishwaji wa mabaraza hayo ya watoto wenye ulemavu na akashauri yawepo sehemu mbalimbali ili watoto hao waweze kupata nafasi ya kupaza sauti zao.

“Watoto wenye ulemavu wako sehemu mbalimbali, ni vyema mabaraza haya yakawepo sehemu nyingi ili watoto hawa waweze kupata nafasi ya kujieleza na kusikilizwa ili wasaidiwe.

“Pia ni vyema maafisa wanaohusika moja kwa moja na watoto hawa wakaangalia njia sahihi za kuzitatua changamoto zao ili nao waweze kuishi maisha mazuri. Lakini noamba niseme tu kwamba, jukumu la kuwasaidia watoto hawa lisiachwe kwa serikali pekee, tukitegemea tu bajeti kutoka serikalini ndiyo iwatatulie watoto hao changamoto, hatutafaniwa.

“Kila mmoja kwa nafasi yake aangalie jinsi anavyoweza kuwasaidia kupata mahitaji yao ya msingi. Hivi ni kiasi gani cha pesa tunatumia katika mambo ya maharusi na starehe nyingine? Kwa nini tusitenge pesa kwa ajili ya kuwasaidia watoto hawa? Tushirikiane katika hili,” alisema Milinga.

Akiizungumzia semina hiyo, mratibu wa mpango wa kuwasaidia watoto wenye ulemevu kutoka FPCT, Lucas Mhenga alisema watoto walioshiriki walifarijika sana na walitumia fursa hiyo kueleza changamoto zao wakiamini watasaidiwa.

 “Ilikuwa ni semina yenye mafanikio, watoto walipata nafasi ya kueleza changamoto zao lakini kile kitendo cha viongozi wa serikali kuacha majukumu mengine na kutumia muda wao kuwasikiliza, kimewapata faraja kubwa.

 “Tunaamini yale waliyoyaongea yatafanyiwa kazi ili watoto hawa ambao kwa muda mrefu jamii imekuwa ni kama imewatenga waweze kuishi maisha mazuri kama wanavyoishi watoto wengine,” alisema Mhenga.

Imeandikwa na Amrani Kaima

Comments are closed.