The House of Favourite Newspapers

Watu 90 Wamefariki Baada Ya Feri Kuzama Katika Pwani Ya Kaskazini Mwa Msumbiji

0

WATU zaidi ya 90 wamefariki baada ya feri kuzama katika pwani ya kaskazini mwa Msumbiji, mamlaka za eneo zilisema.

Maafisa katika jimbo la Nampula walisema watu watano wameokolewa kati ya watu 130 wanaoaminika kuwa ndani ya feri hiyo.

Walikuwa wakikimbia mlipuko wa kipindupindu, katibu wa jimbo la Nampula Jaime Neto alisema. Watoto wengi ni miongoni mwa waliofariki, aliongeza.

“Kwa sababu feri hiyo ilikuwa imejaa watu wengi na haikufaa kubeba abiria iliishia kuzama,” alisema Neto.

Feri hiyo inaonekana ilikuwa ikisafiri kutoka Lunga kuelekea kisiwa cha Msumbiji, nje ya pwani ya Nampula.

Mkoa wa Nampula umekuwa miongoni mwa sehemu zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa wa kipindupindu ambao umeenea katika mataifa kadhaa kusini mwa Afrika tangu Januari mwaka jana.

Kulingana na Unicef, mlipuko wa sasa ndio mbaya zaidi katika miaka 25. Tangu Oktoba 2023, Msumbiji imeripoti visa 13,700 vilizothibitishwa na vifo 30.

Kundi la waasi wa Kiislamu katika jimbo jirani la Cabo Delgado limesababisha vifo vya takriban watu 4,000 na kusababisha karibu watu milioni moja kuhama makaazi yao tangu lilipoanza uvamizi wake miaka sita iliyopita.

Kwa takriban miaka 400, kisiwa cha Msumbiji kilikuwa mji mkuu wa Afrika Mashariki ya Ureno, wakati eneo hilo lilikuwa chini ya utawala wa kikoloni.

Kisiwa hiki ni eneo la urithi wa dunia wa UNESCO kwa usanifu wake wa kikoloni na historia ya kipekee kama kitovu cha biashara.

KIJANA AKUTWA na SARATANI ya PUA INAKIMBILA KWENYE UBONGO – ANAPUMULIA MDOMO – ALIA AKISIMULIA…

Leave A Reply