The House of Favourite Newspapers

Wawa, Morad wafanya mazoezi bwawani wamzuie Donald Ngoma 

0

Wilbert Molandi,

Dar es Salaam

KATIKA kuhakikisha wanapunguza makali ya straika wa Yanga, Donald Ngoma, Azam FC iliwatenga mabeki wa timu hiyo na kuwapa programu ya mazoezi maalum.

Safu hiyo ya ulinzi wa kati ya Azam inaundwa na Pascal Wawa, Said Morad, David Mwantika, Racine Diouf na Aggrey Morris ambaye amerejea kutoka katika majeraha ya goti.

Azam na Yanga, leo Jumamosi zinatarajiwa kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Benchi la ufundi la Azam, katika mazoezi ya juzi Alhamisi jioni, liliwatenga mabeki hao na kupewa mazoezi kwenye bwawa la kuogelea lililopo kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo Azam Complex, Chamazi.

Katika bwawa hilo, mabeki hao walitakiwa kuchezea mipira kwenye bwawa wakiwa wamesimama, mazoezi yaliyosimamiwa na Kocha Mkuu wa Viungo, Adeian Dobre.

Katika hatua nyingine, kocha msaidizi wa timu hiyo, Mario Marinica, alisema hawana hofu dhidi ya Yanga katika mchezo wa leo kutokana na maandalizi ya kutosha waliyoyafanya chini ya Kocha Mkuu, Stewart Hall.

“Tumecheza na Yanga mara nne msimu huu kwenye michuano tofauti, hawajaweza kutufunga mchezo hata mmoja, uliona kilichotokea kwenye mchezo wetu wa mwisho Yanga? Walizawadiwa penalti ambayo haikuwa halali.

“Hata katika Kombe la Mapinduzi walipewa bao la kusawazisha ambalo halikuwa halali kwani mpira haukuvuka mstari, tena tulikuwa pungufu baada ya Bocco (John) kupewa kadi nyekundu,” alisema Mario.

Leave A Reply