The House of Favourite Newspapers

Wawili kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Quran Afrika

Mstahiki Meya  wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaulembo (kushoto) akikabidhi bendera ya Taifa ili kuiwakilisha nchi katika mashindano  ya 19 ya kusoma na kuhifadhi Quran tukufu Afrika.

 

Watanzania wawili wamekabidhiwa bendera ya Taifa ili kuiwakilisha nchi katika mashindano makubwa ya 19 ya kusoma na kuhifadhi Quran tukufu Afrika yatakayofanyika nchini.

Akikabidhi bendera hiyo Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaulembo, kwa wawakilishi pekee ambao ni Shujaa Sulemani kutoka Morogoro na Mbwana Dadi kutoka Pemba amesema kuwa, imezoeleka mara nyingi bendera yetu wanakabidhiwa timu za mpira, lakini leo imekuwa tofauti kwa vijana hawa kupata fursa adhimu kama hiyo.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kufika uwanja wa taifa kwa wingi  Mei 27, mwaka huu kushuhudua mashindano hayo ambapo hakuna kiingilio chochote na mgeni rasmi anatarajia kuwa ni Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa.

Kwa upande wake msimamizi wa mashindano hayo Sheikh Nurdeen Kishk amesema kuwa washiriki wamepatikana kihalali kutoka maeneo yote ya Tanzania kwani ulifanyika mchujo bila upendeleo.

Aliongeza kuwa mashindano hayo yatashirikisha nchi 16 kutoka Bara la Afrika huku kuanzia leo wakitarajia kupokea washiriki na wageni kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Uingereza, Uganda, Afrika Kusini, Saudi Arabia, Omani na Kenya.

Naye Rais wa taasisi hiyo Sheikh Sharif Abdulkadir  ameipongeza Serikali kwa kitendo cha kulinda amani ya nchi kuonesha ushirikiano kuanzia hatua ya mwanzo hadi sasa kwani bila amani huwezi kuandaa mashindano kama hayo na kupata washiriki kutoka nchi tofautitofauti kuja kushiriki.

Comments are closed.