The House of Favourite Newspapers

Wazazi Tumsaidie Rais Magufuli Kuhusu Elimu Bure

Rais Dk. John Pombe Magufuli.

NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kuandika makala haya kwenye safu hii leo.

Hakuna anayebisha kwamba uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli wa kutoa elimu ya msingi hadi sekondari bila malipo kuanzia Januari 2016, umekuwa ni ukombozi mkubwa kwa watoto ambao wazazi wao au walezi hawana uwezo.

 

Sera ya elimu bila malipo ambayo Rais Magufuli ameileta imeondoa ada na michango mingi ambayo wanafunzi walikuwa wakidaiwa na walimu wao kwenye shule nyingi hapa nchini.

Michango hiyo ilikuwa kero kubwa kwa wazazi na walezi na hata kwa wanafunzi wenyewe kwani walikuwa wakisumbuliwa na kuharibu mpangilio wao wa kusoma na matokeo yake baadhi ya wanafunzi wa elimu ya msingi walikuwa wakishindwa kuendelea na masomo ya sekondari.

 

Serikali ilianza kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 18 kila mwezi kuanzia Januari 2016 hadi kufikia shilingi bilioni 23.8 kwa mwezi kugharamia elimu ikiwa ni pamoja na mitihani na michango mbalimbali ili watoto wote hapa nchini wapate elimu bila vikwazo vyovyote kama ufunguo wa maisha.

 

Hakuna atakayebisha nikisema kwamba mpango huo wa elimu bila malipo umeongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kujiunga na elimu ya msingi karibu kila shule ya msingi hapa nchini lakini pia wanafunzi wa kujiunga na elimu ya sekondari, imeongezeka mara dufu.

 

Kwa upande wa jamii ambazo zilikuwa zikiwarubuni watoto wao wasiendelee na masomo kutokana na kushindwa kuwahudumia na badala yake kutaka kuwaoza (wale wa kike), naamini kwa kutolewa elimu bila malipo kutafanya wengi kuwahimiza watoto wao kufanya bidii katika masomo yao.

 

Ukweli ni kwamba kitendo cha kuwatoza tozo mbalimbali wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ni kitendo kibaya kilichokuwa kikishusha morali wa wanafunzi, kwani wengine walikuwa wakirudishwa nyumbani kwa kukosa fedha za michango.

 

Kitendo kile kilikuwa kikisababisha taifa kurejea nyuma kielimu badala ya kusonga mbele na kuwa nyuma katika mapambano ya adui ujinga ambaye hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa akikazana kwamba tupambane naye.

 

Naamini Watanzania wote tunaunga mkono agizo la Rais Magufuli alilolitoa wiki iliyopita la kuchukuliwa hatua viongozi na watendaji wa serikali waliorejesha michango shuleni kinyume cha sheria kwani walifanya hivyo makusudi huku wakijua kwamba serikali imekataza kufanya hivyo.

 

Ni wajibu wa wananchi wote sasa kuwa macho na mtu yeyote ambaye atafanya ujanja wa kuingiza michango kwenye shule zetu kwa sababu mtu kama huyo bila shaka atakuwa na nia nyingine ya kuhakikisha mkakati wa wanafunzi wetu kusoma bila bugudha zikifeli.

 

Kujihakikishia kuwa agizo la Rais Magufuli linatekelezwa ni juu ya wazazi na walezi na wanafunzi, viongozi wa serikali hasa ngazi ya mtaa, kijiji au kata kuwa na mshikamano kupitia kamati za shule kuwa macho katika suala lolote linalogusa michango kwenye shule zetu.

 

Ni imani yangu kwamba kama wote tutakuwa macho, hakuna anayeweza kuendeleza ukiukwaji huu wa sheria na taratibu zilizowekwa na viongozi. Hili linawezekana na cha msingi ni kwa watu wote kuwa macho dhidi ya wahujumu hao wa elimu kwa watoto wetu. Nilisikia kuna baadhi ya walimu walikuwa wakiwatoza fedha watoto nje ya shule zao ili wasigundulike wakidai wanawapa elimu ya ziada.

 

Nihimize jamii kwa kuieleza kwamba huu sio wakati wa kurejesha michango bali ni wakati wa kuongeza miundombinu ili kukabiliana na idadi kubwa ya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari nchini mwetu.

Najua kuna changamoto nyingi kwa walimu wetu lakini huu ndio wakati wa kukabiliana nazo. Tunajua walimu wanadai malimbikizo ya marupurupu yao mbalimbali lakini hilo Rais Magufuli ameliona na ameshasema atalitatua.

Changamoto nyingine ni uhaba wa walimu, hivyo serikali inatakiwa iongeze walimu, miundombinu ya madarasa pamoja na madawati, mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu Watanzania wote chini ya uongozi wa viongozi wa elimu chini ya Waziri wa Elimu, Joyce Ndalichako.

 

Sidhani kama hilo litahitaji msaada wa wafadhili kwa sababu baadhi ya viongozi wa shule wameweza.

Tukifanya hivyo, naamini ndani ya miaka kumi ijayo adui ujinga atakuwa amepigwa na vijana wetu wengi watakuwa na upeo wa elimu ya sekondari.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

NAPASUA JIPU UWAZI | ERIC SHIGONGO | DAR ES SALAAM

Comments are closed.