The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-23

0

ILIPOISHIA WIKIENDA 

 Kama itakuwa hivyo, nilijiambia taarifa itafikishwa kwa waziri mkuu usiku uleule na huenda nikachukuliwa hatua.

 Hatua pekee ambayo ningechukuliwa ni kutumwa polisi waje wanikamate nyumbani kwangu na kesho asubuhi rais akishafahamishwa nilichokifanya atanifuta kazi. 

SASA ENDELEA… 

Wazo hilo ndilo lililonitia hofu, kufukuzwa kazi, kuumbuka na mwisho wake kushtakiwa kwa kumuwangia waziri mkuu na kuweka kinyesi changu mbele ya mlango wake.

 Wakati nayawaza hayo nilikuwa nimeshalitoka eneo la Masaki, ghafla nikaona polisi walioegesha gari lao pembeni mwa barabara wakinipungia mkono kunisimamisha.

Sikuweza kujua kuwa wale polisi walikuja kunitega mimi pale au walikuwa wamenitilia mashaka. Lakini katika hali yoyote ile kile kitendo tu cha kunikuta waziri mzima niko uchi wa mnyama ndani ya gari nikiwa na mkoba wenye vitu vya ajabu, lilikuwa jambo ambalo lingewashangaza polisi hao.

Kwa vyovyote vile isingenipasa kusimama japokuwa polisi hao tayari walikuwa wameninyooshea mikono ya kunisimamisha.

 Taa za gari langu zilikuwa zikiwamulika na niliwaona wakiwa pembeni mwa barabara. Sikuwa na sababu yoyote ya kujifanya sikuwaona.

Nikapunguza mwendo nikijifanya kama nataka kusimama, niliwapita kidogo na kuielekeza gari langu pembeni mwa barabara. Wakati polisi hao wakiwa wamedanganyika kudhani kwamba ninasimamisha gari baada ya kuwapita, nikatia gea na kuongeza mwendo.

Kitendo hicho kiliwaudhi polisi hao na kuwapa mashaka. Kwa kutumia kioo cha kutazamia nyuma niliwaona wakikimbilia kwenye gari lao lililokuwa pembeni mwa barabara wakaliwasha na kuanza kunifukuza.

Wakati huo nilikuwa mbali. Nikakata kona kushoto ili kuwakwepa. Nilipokwenda mbele kidogo nikakata tena kushoto na kuingia mtaa mwingine.

Wakati naingia mtaa huu sikuliona gari hilo la polisi nyuma yangu, sasa nikakata tena kulia ili kuwapoteza zaidi.

 Niliona kichochoro kilichokuwa kiza upande wangu wa kushoto nikaliingiza gari hilo na kulisimamisha. Nilijua kwa vyovyote nilikuwa nimeshawapoteza polisi hao na wasingeweza kujua kuwa nilisimama mahali hapo.

Baada ya kulisimamisha gari nilivaa nguo zangu ndani  ya gari. Wakati namaliza kuvaa nililiona gari la polisi likipita kwa kasi nyuma yangu. Kama wangekata kona na kuingia katika kile kichochoro nilichokuwepo wangeniona na kunikamata. Lakini kwa bahati njema hawakutazama upande huo.

Nikaona nisingeweza kulitumia tena lile gari kwani ningeweza kukamatwa nalo. Sikujua hao polisi wangeishia wapi na kwa vile walikuwa katika doria, kwa vyovyote vile, ningeweza kukutana nao.

Isitoshe polisi wanapokuwa na mashaka na gari lililowatoroka wana tabia ya kupigiana radio call. Wanaweza kuwa wamewapigia wenzao waliokuwa katika doria upande mwingine na kuwaagiza kwamba watakapoliona gari hilo walikamate.

Nikaliacha gari hilo na kutembea kwa miguu nikiwa na mkoba wangu. Licha ya kwamba ulikuwa usiku mwingi, mitaa ya Jiji la Dar ilikuwa bado ina pilikapilika.

 Nilikwenda katika kituo cha teksi nikakodi teksi iliyonipeleka karibu na nyumba yangu.

 Sikutaka kufika nyumbani kwangu kabisa ili dereva wa teksi huyo asigundue kuwa ninaishi katika nyumba hiyo ambayo ilikuwa ikifahamika kuwa ni nyumba ya waziri.

 Mlinzi wa geti la nyumba yangu alinifungulia geti nikaingia ndani. Bila shaka hata yeye alishangaa kuniona sikuwa na gari na nilikuwa nikitembea kwa miguu usiku huo.

Nilikwenda kubisha kwenye dirisha la chumba changu. Mke wangu akaamka na kuniuliza:

“Nani…Meshack?”

“Ndiyo nifungulie,” nikamwambia.

Baada ya dakika tatu hivi mlango wa mbele ukafunguliwa, nikaingia ndani.

 Nilijua kuwa mke wangu asingeniuliza kuhusu gari kwa sababu kwa mawazo yake alijua nilirudi na gari hilo na nililiweka kwenye banda.

 Kama angejua kuwa sikuwa na gari hilo, angenisumbua kwa maswali na sikuwa na jibu la kumpa.

 Kama atajua ni hapo kutakapokucha, nitajua jinsi ya kumueleza, nilijiambia.

 Hata hivyo, nilikuwa na hakika kwamba gari lile lingelala pale hadi asubuhi ambapo ningemtuma dereva wangu alifuate.

“Ndiyo unarudi kutoka ofisini kwako?” Mke wangu akaniuliza tulipokuwa sebuleni. Alikuwa akinitazama kwa mashaka mashaka.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu. 

Leave A Reply