The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-34

0

ILIPOISHIA IJUMAA:
“Amejifungua salama?”
“Amejifungua salama.”
“Ni sasa hivi au ni muda uleule mliofika?”

“Tulipofika hakukaa sana, akaingizwa kizimbani.”
“Kuna kipindi nilipiga simu lakini haikupokelewa.”
“Nilikuwa nikishughulika na yeye.”
“Sawa, basi nitakuja kuwaona.”
SASA ENDELEA…

Muda wangu wa kutoka kazini ulipowadia niliondoka ofisini kwangu, dereva wangu akanirudisha nyumbani. Nilioga, nikabadili nguo na kutoka tena, sasa kwa kutumia gari binafsi.

Nilikwenda hospitalini alikojifungua mke wangu huko Mikocheni. Nilipofika nilifanikiwa kumuona mke wangu akinyonyesha kichanga chetu. Nilipata furaha sana kukiona kitoto kidogo cheupe chenye nywele laini kama za singa.

Nilimpa hongera mke wangu kwa kunizalia mtoto wa kiume kama ambavyo nilitarajia.
Nilipompa hongera mke wangu alitabasamu. Nikahisi kwamba vile vituko vya ujauzito vya kununanuna ovyo vilikuwa vimekwisha baada ya kujifungua. Sikuwahi kuona tabasamu lake kwa miezi kadhaa. Jioni ile ndiyo nililiona. Lilikuwa tabasamu la dhati lililonifariji.

“Ana uzito wa kilo ngapi?” nikamuuliza huku nikiketi kwenye kistuli kilichokuwa karibu na kitanda.

“Ana kilo tatu,” mke wangu akanijibu huku akiendelea kutabasamu.
“Umemzaa na uzito mzuri.”
“Ila madaktari wameniambia ana upungufu wa vitamin C, nitaendelea kuwa hapa hospitali.”

“Kwa nini akose vitamin C?” nikamuuliza kwa pupa.
“Hebu nielewe babake, si kwamba amekosa vitamin C bali ana upungufu wa vitamin C,” mke wangu akaniambia kwa msisitizo kama vile anamwambia mtoto mdogo asiye na akili.

Sikuchukulia ni mambo ya mapenzi!
“Nilivyoelewa mimi ni kwamba hana vitamin C ya kutosha, siyo kwamba hana kabisa.”
“Kwa hiyo itakuwaje?” nikamuuliza.

“Wameniambia niendelee kukaa hospitalini angalau kwa siku tatu, asubuhi nitakuwa ninatoka naye nje ili apate mwanga wa jua kidogo.”
“Ndiyo wamekwambia hivyo?”
“Ndiyo.”

“Basi hakuna tatizo. Tunachotaka sisi ni uzima tu, unaweza kuendelea kukaa kisha wataniletea bili yao.”
“Mpe jina basi au nimpe mimi?”
“”Umpe wewe wakati mimi baba yake nipo.”
“Mpe basi. Utamuita nani?”

“Sikuwa nimepanga jina ila mpaka kesho asubuhi nikija kuwatazama nitakuja na jina lake.”
“Nikupe umshike kidogo.”

“Nipe.”
Mama yake alijaribu kumuondoa kwenye ziwa lakini kichanga kilikuwa kimeng’ang’ania.
“Basi kaache kanaweza kulia,” nikamwambia mama yake.
“Kanapenda kunyonya kweli, tangu nijifungue kananyonya tu.”
“Kaache kanyonye, hakajashiba bado.”

“Kikishiba kitalala nipumzike kidogo.”
“Namshukuru Mungu mke wangu umezaa salama tena umenizalia baba yangu.”
“Mungu akinijalia tena na mimi nitamzaa mama yangu.”
“Ni sawa. Umeanza mume halafu anafuatia mke.”
Niliendelea kuongea na mke wangu hadi ikapita saa nzima. Nilipoona jua linakuchwa nikamuaga mke wangu.

“Utakwenda kula wapi usiku?” akaniuliza.
“Nitakula hotelini.”
“Sawa, basi ni hapo kesho asubuhi utakapokuja.”
Nikamuaga mama, mke kisha nikatoka. Sikuwa na tatizo lolote na pale hospitali kwani palikuwa na kila kitu ambacho mgonjwa au mwanamke aliyekwenda kujifungua atahitaji.

Mgonjwa alikuwa akihudumiwa kila kitu kuanzia chakula, sabuni, shuka za kujifunika na mahitaji mengine. Palikuwa ni mahali pazuri kwa mgonjwa lakini gharama yake ilikuwa kubwa.

Waliokuwa wakitumia hospitali ile walikuwa watu wenye vipato vikubwa kama sisi mawaziri na watu wengine waliojimudu kimaisha.
Breki yangu ya kwanza ilikuwa ni kwenye hoteli moja ambako mara kwa mara nilikuwa nikikutana na marafiki zangu wa zamani, nikimaanisha watu niliosoma nao chuoni ambao kwa wakati ule miongoni mwao walikuwa ni waajiriwa serikalini na wafanya biashara.

Nilipofika hapo hoteli nikakutana na rafiki yangu mmoja ambaye si tu nilisoma naye Chuo Kikuu cha Mlimani bali pia tulitoka mkoa mmoja. Yeye alikuwa mfanyabiashara.
Tukazungumza sana. Yule bwana aliagiza chakula akaniagizia na mimi. Nikapata hapohapo mlo wa usiku tena wa bure.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.

Leave A Reply