The House of Favourite Newspapers

Kamwelwe Aagiza Kukamatwa kwa Anayeendesha Aviation TV

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania, Isack Kamwelwe ameagiza anayeendesha mtandao wa ATCL Aviation TV kukamatwa kwa kutangaza kuwa ndege nyingine mpya aina ya Dreamliner inakuja nchini wakati si kweli. Kamwelwe ameeleza hayo leo Oktoba 24, 2019 jijini Dar es Salaam katika kongamano la Tehama lililowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo kujadili mchango wake kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda.

Amesema kila jambo lina mamlaka zake za kutangaza na kama ni suala la ndege, wizara yake ndio ina dhamana ya kutangaza. Amesema ameliuliza Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) wakamueleza kuwa hawakifahamu chombo hicho, nao pia wanashangaa.

“Nimeagiza atafutwe nimemwambia na Waziri wa Mambo ya Ndani (Kangi Lugola) kuangalia sheria ya kumshtaki. Kama hakuna sheria tutamsumbua tu mpaka wenzake wamuonee huruma,” amesema Kamwelwe. Amesema imefikia hatua vyombo vya habari vinatangaza kifo cha mtu, kusisitiza kuwa Taifa lina maadili yake na hali hiyo haitaachwa iendelee.

Comments are closed.