The House of Favourite Newspapers

Waziri Ummy atahadharisha juu ya homa ya manjano

0

1.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akifafanua jambo baada ya kusoma taarifa yake kwa wanahabari (hawapo pichani).

2

Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya na Ubora, Dk. Fauster Mosha (kulia) akitoa ufafanuzi wa jambo.

3Baadhi ya viongozi wa wizara ya afya wakiwa katika mkutano huo.
4Wanahabari wakichukua matukio kwenye mkutano huo.
5 Sehemu ya wanahabari waliohudhuria.

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,  leo ametoa tahadhari juu ya ugonjwa wa homa ya manjano ulioingia nchi ya jirani ya  Kenya ambapo tayari wagonjwa wawili walithibitika kuwa na ugonjwa huo na mmoja wao akiripotiwa kufariki dunia.

Hayo ameyasema leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wanahabari juu ya kuchukua tahadhari ya mlipuko huo wa ugonjwa wa manjano kabla ya kuingia hapa nchini.  Alisema  wagonjwa hao walikuwa na historia ya kusafiri kutoka nchini Angola ambapo kuna mlipuko wa ugonjwa huo.

Amesema, taarifa zinaonesha kuwa nchini Angola hadi kufikia Machi 9 mwaka huu kulikuwa na jumla ya wagonjwa 813 ambapo vifo  vilikuwa watu 138 na wengine 65 wakithibitishwa kimaabara.
Aidha amewatahadharisha wananchi wote  kutambua na kujikinga na ugonjwa huo hasa  wananchi walio katika mikoa ya jirani ambayo inapakana na nchi ya Kenya pamoja na maeneo yote ambayo watu huingilia nchini kwenye mipaka ya nchi kavu, maziwa, viwanja vya ndege na bandarini.

Mwalimu alimtaja mbu anayeeneza virusi vya uginjwa huo wa manjano kuwa ni ‘Aedes’ ambapo pia dalili zake ni homa, kuumwa na kichwa, maumivu ya misuli, mwili kutetemeka, kupoteza hamu ya chakula, kuhisi kichefuchefu, kutapika, mwili kuwa na rangi ya manjano hata kutokwa na damu sehemu za wazi kama mdomoni, puani na machoni.

Alisema wakati mwingine damu huonekana kwenye matapishi na kinyesi, figo kushindwa kufanya kazi huku kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa huo kikiwa ni kati ya siku tatu hadi sita baada ya kuambukizwa.
Vilevile alieleza ripoti ya wiki ya mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini kuanzia Machi 14 hadi 20,  mwaka huu kuwa takwimu zinaoonesha jumla ya wagonjwa walioripotiwa ni 738 na vifo 16 huku mikoa 13 ikiwa na wagonjwa wa kipindupindu ambapo iliyoongozwa ni mkoa wa Manyara (110) ukifuatiwa na Mwanza (92) na mikoa mingine.
Hata hivyo, alisema wataalam kutoka ngazi ya taifa, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani  na serikali za mitaa (Tamisemi) wapo katika mikoa ya Dodoma, Mara, Mwanza, na Morogoro wakishiriki katika mikakati ya kuthibiti ugonjwa huo hasa katika ngazi ya jamii kwa kushirikisha viongozi wa kata na vijiji na kutoa elimu juu ya ugonjwa wa kipindupindu.

Na Denis Mtima/Gpl

Leave A Reply