The House of Favourite Newspapers

‘WAZUNGU WATATOWEKA WAKIMBIZI WAKIFURIKA ITALIA’

MWANASIASA wa chama cha Northern League cha Italia, Attilio Fontana, amewataka wananchi wenzake kuamua iwapo wanataka watu wa ‘ngozi nyeupe’  (Wazungu) waendelee kuwepo au watoweke.

Fontana ameyasema hayo  Jumapili iliyopita wakati wa kampeni kuelekea katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini humo Machi mwaka huu na ambapo hivi sasa kuna wimbi kubwa la Wafrika ambao wamekuwa wakihamia  barani Ulaya.

“Tunalazimika kuamua asili yetu, iwapo Wazungu waendelee kuwepo au watoweke kutokana na wimbi la Waafrika kuingia nchini mwetu,” alisema Fontana anayegombea ugavana wa jimbo la Lombardy.

Baadhi ya mamia ya wakimbizi wa Afrika wakiwa barani Ulaya.
Mwanasiasa Attilio Fontana aliyelaumu uhamiaji wa Waafrika nchini Italia.
Ofisa usalama wa Italia akiwadhibiti wakimbizi kutoka Afrika.

Fontana alisema hayo Jumapili akisisitiza kwamba hilo halikuwa suala la kuchukia watu wa rangi au mataifa mengine, bali suala la uamuzi na lenye kueleweka.

Zaidi ya watu 600,000 wameingia nchini Italia tangu mwaka 2014, wengi wao wakiwa wameokolewa baharini katika majaribio ya kuingia barani Ulaya.

Wakimbizi wa Afrika waliookolewa baharini kwa kutupiwa maboya.

Akiwa anashutumiwa sehemu mbalimbali kwa kauli hiyo, Fontana alisema jana kwamba hilo lilitokana na ulimi wake kuteleza, lakini, hata hivyo, alijihami kwa kusema kwamba katiba ya nchi yake ilikuwa ya kwanza kuzungumzia ‘rangi’ tofauti za watu.

Waziri mkuu wa zamani, Silvio Berlusconi, wa chama chenye msimamo  wa kati-kulia cha Forza Italia, ambacho kimeungana katika uchaguzi huo na chama cha Northern League, alisema kauli za Fontana zimekuwa za ‘bahati mbaya’.

“Utamaduni wetu, jamii yetu, mila zetu na aina ya maisha yetu, vinatishiwa.  Uvamizi dhidi ya vitu hivi hivi sasa kweli unakuja,” alisema na kuongeza kwamba rangi ya ngozi si tatizo, lakini hatari hiyo ipo kweli,  kwani historia iliyochukua mamia ya miaka inaweza kutoweka.”

 

WALUSANGA NDAKI/MITANDAO/MASHIRIKA

Comments are closed.