The House of Favourite Newspapers

Wema Afichua Siri mpya na Mondi

HATA kama mtu umeachana naye kwenye uhusiano wa kimapenzi, haikatazwi kuzungumzia au kukumbukia nyakati nzuri na mbaya mlizopitia enzi za uhai wa penzi lenu.  Hicho ndicho kinachojiri kwa staa mkubwa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu ambaye ameamua kufichua siri mpya ambayo hajawahi kuisema juu ya zilipendwa wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Wema au Tanzanian Sweetheart ameshindwa kuendelea kukaa nalo moyoni na kuamua kutoa siri ambayo watu wengi walikuwa hawaijui kuhusu yeye na Diamond au Mondi.

WEMA NA GAZETI LA AMANI

Katika mahojiano maalum na Gazeti la Amani, Wema ambaye penzi lake na Mondi lilikuwa gumzo ndani na nje ya Bongo yapata miaka mitano iliyopita, ameweka wazi jinsi ambavyo hajawahi kuwapenda wapenzi wa waliofuata baada yake kwa mwanamuziki huyo mkubwa barani Afrika kwa sasa. Wema amefunguka mambo mengi ambayo ni maisha yake ya sasa na mabadiliko ambayo amekutana nayo kwenye mwili wake baada ya kupungua.

MAHOJIANO DAKIKA 30

Msikie mwenyewe akitiririka kwenye mahojiano hayo yaliyochukua takriban dakika thelathini na mwandishi wetu;

Amani: Wema kuna tetesi kuwa kwa sasa huna uhusiano mzuri na familia Diamond, hili likoje?

Wema: Mimi? (kwa mshangao) kwa upande wangu mimi nafikiri sina tatizo lolote lile na watu hao unaowasema, labda kwa upande wao, lakini mimi niko sawa kabisa.

Amani: Mbona hata siku ya birthday yako (Septemba 28), hakuna mtu wa familia ya Mondi aliyekuposti kwenye kurasa zao za Instagram kama zamani, kulikoni?

Wema: Jamani kumposti mtu ni chaguo la mtu na siyo vinginevyo, kwa hiyo siyo kitu cha kumlaumu mtu au kumuuliza kwa nini.

Amani: Au tatizo linaweza kuwa upande wako kwa kumsapoti Harmonize ambaye ameondoka kwenye lebo yao wa Wasafi Classic Baby (WCB)?

Wema: Jamani, mimi Harmonize ninaukubali muziki wake siku nyingi sana, siyo jana wala leo.

Amani: Kwa hiyo una shida na Mondi?

Wema: Hapana, sina tatizo naye.

Amani: Unaweza kukumbuka nyimbo ambazo Mondi alikuimbia wakati mapenzi yenu yakiwa shatashata?

Wema: Ni nyingi mno, tena sana.

Amani: Kwa nini unasema ni nyingi?

Wema: Kwa sababu alikuwa akiniambia siku zote, ili aimbe wimbo mkali lazima anifikirie ndiyo anatoa wimbo na unapendwa sana.

Amani: Kwa upande wako ni mwanamke gani ungependa awe na Mondi kati ya yote waliopita au aliye naye kwa sasa (Tanasha Donna)?

Wema: Hakuna mwanamke wake ambaye ninampenda, nisiwe mnafiki kabisa mimi.

Amani: Kwa nini?

Wema: Unajua Nasibu (Mondi) ni mtu ambaye nimekaa naye sana kama mpenzi ‘so’ siwezi kusema eti ninampenda mwanamke wake, hiyo itakuwa ni unafiki kabisa kwangu. Yaani siwezi kumpenda mwanamke wake yeyote hadi nakufa.

Amani: Hivi na yeye anajua hilo?

Wema: Itakuwa anajua.

Amani: Haya, poa Wema ninashukuru.

Wema: Asante, karibu tena.

WEMA NA MONDI

Katika kipindi cha miaka kadhaa ya penzi lao, Wema na Mondi waliachana na kurudiana mara tatu.

Mwaka jana, baada ya Mondi kuachana na mzazi mwenzake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ alidaiwa kurudiana na Wema baada ya picha na video zao za kimahaba kusambaa mitandaoni.

Hata hivyo, kwa sasa Wema ana mpenzi wake mpya ambaye amekuwa akimficha kuhofia nyakunyaku wa mjini, huku Mondi akilea mwanaye mchanga aliyezaa na Tanasha hivi karibuni.

Stori: Imelda Mtema, Amani

Comments are closed.