The House of Favourite Newspapers

Wema: Mniache na Whozu Wangu! Nisije Kujinyonga Kama Katibu wa Masanja

0
Wema Isaac Sepetu.

Wema Isaac Sepetu na Whozu; ni mastaa wa Bongo ambao wanazungumzwa zaidi kutokana na penzi lao kuzidi kung’ara kila kukicha huku mrembo huyo akiomba aachwe na kuahidi kuwa kama katibu aliyejinyonga, IJUMAA lina ripoti kamili ya penzi hilo.

 

WEMA KAMA KATIBU

Wema anasema kuwa, pamoja na kwamba hakujiua kwenye uhusiano wake wa kimapenzi huko nyuma likiwemo penzi la msanii Diamond Platnumz na wengineo, lakini safari hii akiachwa na Whozu, atakuwa kama MC Joas aliyekuwa Katibu wa Kanisa la Feel Free Church la Masanja Mkandamizaji ambaye alidaiwa kujinyonga hivi karibuni, kisa kikidaiwa ni kukataliwa penzi na mke wa Masanja.

 

Wema anasema kuwa, kama akiachwa na Whozu, basi watu wakaribie msibani kwa ajili ya kumzika kwa sababu jamaa huyo amemuheshimisha mno.

Wema Isaac Sepetu na Whozu.

Penzi la Wema na Whozu limechipuka kipindi cha hivi karibuni na limeanza kuteka mazungumzo mtandaoni.

Wema anasema kuwa, pamoja na kwamba watu wanambeza kuwa, lakini anataka aachwe na maisha yake kwani ukweli ni kwamba amezama kabisa kwenye dimbwi la mahaba na ana furaha mno.

 

WEMA NA WHOZU HAWAKUANZA LEO

Taarifa ambazo Gazeti la IJUMAA linazo ni kwamba, penzi la Wema na Whozu halikuanza leo wala jana kwani walijificha kwenye mwavuli wa marafiki, ila walikuwa wakifanya kwa siri kabla ya kuamua kujitokeza hadharani kama wapenzi baada ya Whozu kuachana na mzazi mwenzake, Tunda.

 

“Kwa muda mrefu nimekuwa sina raha. Nimekuwana huzuni, nimekuwa nikilia, lakini tangu nilipokutana na Chibaba wangu (Whozu) nimekuwa na raha na amekuwa akiweka tabasamu kwenye uso wangu,” anasema Wema.

 

Wema na Whozu walionekana wakijivinjari pamoja, wakikumbatiana, kudensi pamoja na hata kubusu mbele ya kamera kabla ya Wema kueleza jinsi alivyozama kwenye mahaba anayopewa na jamaa huyo.

 

WHOZU AMFANYIA WEMA KUFURU

Wema anamtambulisha Whozu kwa uhusika wake mkubwa katika maandalizi ya pati ya kusherehekea siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake hivi karibuni.

 

Kwa mujibu wa Wema, Whozu alimfanyia kufuru kwa kugharamia pati hiyo iliyohudhuriwa na marafiki kadhaa wa Wema.

 

“Asante kwa kila kitu mpenzi wangu. Unaweza kuona hiki ni kidogo, bali hujui tu kina ukubwa gani umegusa moyo wangu,” anasema Wema akimshukuru Whozu.

 

Wema mwenye umri wa miaka 32, anasema kuwa, anasubiri mno tarehe 10 mwezi Machi ufike (mwakani) ili aweze kumfanyia Whozu makubwa katika kumbukizi yake ya kuzaliwa kama njia ya kulipa deni lake kubwa kwake.

Wema anamhakikishia Whozu kuhusu upendo wake mkubwa kwake na kumuombea mema maishani.

 

“Yote tisa, nataka tu ujue unamaanisha ulimwengu kwangu. Na nitaendelea kukuombea kwa Mungu kila siku ya maisha yangu. Baraka zote zije kwako kwa sababu unastahili kila jema katika maisha yako,” anasema Wema.

Wema anaendelea kumuombea Whozu maisha marefu na kudokeza kuwa angependa kuwa naye katika kipindi chote cha maisha alichobakiza duniani.

 

“Umefanya msichana ajihisi amebarikiwa kwa mara nyingine maishani. Kupendwa raha sana. Roho yako nzuri ibarikiwe,” anasema Wema kwa Whozu.

 

Katika jibu lake, Whozu anamhakikishia Wema kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

“Unaweza ukajiona mwenye bahati, lakini nataka ujue mimi ndiye mwenye bahati kuwa Chibaba wako. Nakupenda sana Chimama,” anasema Whozu.

 

WANAUME WA WEMA KABLA YA WHOZU

Kumbukumbu zilizopo kwenye makabrasha ya Gazeti la IJUMAA zinaonesha kwamba Whozu siyo mwanaume wa kwanza kuwa katika maisha ya Wema kwani ana listi ndefu;

 

 

JUMBE, MR BLUE NA TID

Miaka kadhaa kabla ya kukutana na Kanumba, Wema alidaiwa kuwa kwenye mapenzi mfanyabishara aliyejulikana kwa jina la Yusuf Jumbe kisha akatamba na mastaa wakubwa wa muziki wa wakati huo; Mr Blue na TID Mnyama; yule wa Zeze.

 

Hakuna ripoti nyingi kuhusu uhusiano wa Wema na Mr Blue, lakini kwa upande wa TID walidaiwa kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi mwaka 2006 wakati huo Wema akiwa na Taji la Miss Tanzania.

 

STEVEN KANUMBA

Baadaye, Wema alipojiingiza kwenye tasnia ya filamu nchini Tanzania alijikuta mikononi mwa aliyekuwa kinara wa tasnia hiyo, marehemu Steven Kanumba.

 

Miaka kadhaa iliyopita Wema alifichua kuwa marehemu Steven Kanumba ndiye alikuwa mpenzi wake wa kwanza na wa ukweli.

Wema alisema alichumbiana na Kanumba kwa muda kabla ya jamaa huyo kukumbana na kifo siku ile ya Aprili 7, 2012; yapata miaka kumi iliyopita.

 

DIAMOND PLATNUMZ

Wema na Diamond Platnumz au Simba wa Tandale walichumbiana kwa kipindi kirefu kabla ya mapenzi yao kufika kikomo mwaka wa 2014 huku wakipita kwenye vipindi vya maji kupwa na kujaa.

Wawili hao ambao walipendana mno walikuwa kwenye mapenzi ya msimu yaliyokumbwa na madai kadhaa ya kuchepuka.

 

Hata hivyo waliendelea kuchumbiana hadi Diamond alipokutana na Zari The Boss Lady na hatimaye kumtema muigizaji huyo.

 

OMMY DIMPOZ

Wema na Ommy Dimpoz walidaiwa kuwa kwenye mapenzi kipindi kifupi baada ya Wema kutengana na Diamond.

Matendo ya wawili hao pamoja na jumbe tamutamu walizoandikiana zilifanya watu kuamini kuwa ni wapenzi.

Hata hivyo, baadaye Dimpoz alikanusha madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Wema akidai kuwa walikuwa wakifanya kazi pamoja katika Wimbo wa Wanjera.

 

LUIS MUNANA

Wema alikutana na mwanamitindo wa Namibia, Luis Munana takriban mwaka moja baada ya kutengana na Diamond.

Baada ya kipindi kifupi alitengana naye kwa sababu hakuweza kumudu uhusiano wao wa mbali na baadaye kisha akatua kwa Iddris Sultan.

 

IDRIS SULTAN

Wema alichumbiana kwa muda na Iddris Sultan aliyekuwa ametoka kuchota  kabla ya kutengana kwao mwaka wa 2016.

Licha ya mapenzi yao kugonga mwamba miaka mingi iliyopita huku Wema akidaiwa kunasa ujauzito wa jamaa huyo na kuharibika, wawili hao wamebaki kuwa marafiki.

 

CHAZ BABA

Wema hakuishia hapo kwani alizama kwenye mahaba niue na staa wa muziki wa Dansi Bongo, Charles Gabriel ‘Chaz Baba’.

Ni katika kipindi hicho ambapo familia ya Wema iliona ili kumnusuru ni bora akaishi na kusoma kwa dada yake nchini Marekani hivyo kuvunja penzi lake na Chaz Baba.

 

CALISAH

Wema na mwanamitindo wa Bongo, Calisah walichumbiana kwa muda takriban miaka 6 iliyopita kabla ya mapenzi yao kusambaratika katika njia ya kushangaza.

Wawili hao walitengana baada ya Calisah kudaiwa kuvunjisha video yao chafu kwenye mitandao ya kijamii.

 

NAGARI KOMBO

Mwingine anayetajwa kwenye listi ya Wema ukimuacha yule Kigogo wa Wema au CK, ni kijana wa mjini, Nagari Kombo aliyepata umaarufu baada ya kuingia Uwanja wa Taifa (sasa kwa Mkapa) na kumkumbatia staa wa soka wa Brazil, Ricardo Kaka. Hata hivyo, penzi lao halikudumu.

 

SASA AMETULIA NA WHOZU WAKE

Kwa mujibu wa Wema, kwa sasa ametulia tuli kama maji ya mtungi kwa Whozu wake akisubiri kufunga naye ndoa mwakani.

Stori; Mwandishi Wetu, Dar

Leave A Reply