The House of Favourite Newspapers

Wenye Miaka 58 na Zaidi Kupewa Kipaumbele Chanjo ya Corona Kenya

0

Serikali sasa imesema itawapa kipaumbele wale walio na umri wa miaka 58 na zaidi katika shughuli inayoendelea ya kutoa chanjo ya Covid-19.

 

 

Mpango wa awali ulikuwa kuwazingatia mwanzo wahudumu wa afya ,walimu na wale walio katika vikosi vya usalama katika kuwapa chanjo kwa sababu ya mazingira ya kazi zao.

 

 

Lakini Wizara ya Afya sasa inasema uamuzi wa kuwajumuisha wazee katika awamu ya kwanza ulifikiwa baada ya data kuonyesha kuwa watu katika umri huu wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa sugu na wanachangia asilimia 60 ya vifo vilivyorekodiwa nchini.

 

 

Kenya kwa sasa inashuhudia wimbi la tatu la maambukizi ya Corona na idadi ya wanaopatikana na virusi hivyo inazidi kuongezeka kila uchao.

 

 

Tayari hospitali nyingi hazina nafasi katika vitengo vya wagonjwa walio katika hali mahtuti ,ICU hatua ambayo imeilazimu serikali kurejesha tena mpango wa kuwatunza wagonjwa wa Corona majumbani.

 

 

Mwenyekiti wa jopo kazi la utoaji wa chanjo Willis Akhwale amesema uamuzi huo wa serikali unaambatana pia na mapendekezo ya shirika la afya duniani WHO na jopo kazi la kitaifa linaloongoza utoaji wa chanjo.

Leave A Reply