The House of Favourite Newspapers

Winga AS Vita Mlangoni Yanga Kumuondoa Moloko na Skudu Makudubela

0
Kiungo mshambuliaji anayetokea kulia, Elie Mpanzu.

IMEFAHAMIKA kuwa, Yanga wameifuata Klabu ya AS Vita ya DR Congo, kwa ajili ya mazungumzo ya awali kwa ajili ya kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji anayetokea kulia, Elie Mpanzu.

Ujio wa winga huyo huenda ukamuondoa kiungo mmoja wa pembeni wa timu hiyo, katika dirisha dogo la usajili. Mawinga hao ni Jesus Moloko na Skudu Makudubela ambao hawana nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Kocha Muargentina, Miguel Gamondi.

Yanga imepanga kukiimarisha kikosi chao katika dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Desemba 15, mwaka huu kwa ajili ya kujiimarisha zaidi na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, ripoti aliyoikabidhi Gamondi katika Kamati ya Mashindano ya timu hiyo, imependekeza isajili mshambuliaji na kiungo mmoja wa pembeni ambaye anatajwa ni Mpanzu.

Mtoa taarifa huyo alisema tayari Yanga imefungua mazungumzo na uongozi wa AS Vita, kwa ajili ya kununua mkataba wake wa mwaka mmoja alioubakisha katika klabu yake hiyo.

Aliongeza kuwa, kiungo ana uwezo mkubwa wa kucheza winga ya kulia na kushoto, ambaye yeye mwenyewe kiungo huyo anavutiwa kuja kuichezea Yanga baada ya kupata ushawishi kutoka kwa wachezaji wenzake Wakongo ambao ni Maxi Nzengeli, Joyce Lomalisa na Moloko.

“Kamati imepokea ripoti ya mapendekezo ya usajili kutoka kwa kocha ikipendekeza kusajili wachezaj wawili pekee ambao ni mshambuliaji na kiungo mshambuliaji ambaye amepatikana na kuanza mazungumzo ya awali na uongozi wa AS Vita inayommilika kwa sasa.

“Kama mazungumzo yakienda vizuri, basi haraka dili litakamilika ambaye anakuja kuiboresha safu ya ushambuliaji.

“Ujio wa Mpanzu unakuja kumuondoa kiungo mmoja wa pembeni, kutokana na idadi ya wachezaji wa kimataifa kukamilika, hivyo ni lazima aondoke mmoja ili mwingine aingie,” alisema mtoa taarifa huyo.

Yanga kupitia Rais wa timu hiyo, Injinia Hersi Said, alizungumzia hilo la usajili kwa kusema: “Tumepokea tayari ripoti ya kocha wetu Gamondi ambayo imetoa mapendekezo ya kusajili wachezaji katika dirisha dogo.

“Ripoti hiyo tutaifanyia kazi vizuri, kwa kusajili wachezaji wote aliowapendekeza katika dirisha dogo, ili kuhakikisha kikosi chetu kinakuwa imara kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ni michuano mikubwa.”

STORI NA WILBERT MOLANDI

Leave A Reply