The House of Favourite Newspapers

XPENG G3; Gari la Kisasa Lenye Uwezo wa Kujipaki Lenyewe Bila Dereva

0

 

Bila shaka umeshasikia sana kuhusu magari ya kisasa yanayotumia umeme jinsi yalivyokuja kuleta mapinduzi makubwa katika usafiri wa magari duniani. Kama bado hujasikia, ngoja nikudokeze kidogo!

 

Kampuni ya Tesla, ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuzalisha magari yanayotumia umeme badala ya yale yaliyozoeleka, yanayotumia mafuta. Tayari kuna magari ya Tesla Model X, Tesla Model 3, Tesla Model Y, Tesla Model S na kadhalika ambayo yapo sokoni katika nchi zinazoendelea! Hayatumii mafuta kabisa, bali unachaji kwa umeme kama unavyochaji simu yako!

 

Mfumo mzima wa gari unatumia umeme na yanaambatana na teknolojia kubwa ndani yake na hakika yameleta mapinduzi makubwa, yakiwa na sensors za kisasa na uwezo mkubwa wa kumsaidia dereva pale inapotokea dharura.

 

Sasa baada ya Tesla chini ya mgunduzi wake, Elon Musk kuonesha njia, kampuni ya Kichina ya Xpeng, zamani ikifahamika kwa jina la Xiaopeng, imezindua gari lake la kwanza linalotumia umeme, Xpeng G3 ambalo ni kama ‘copy and paste’ ya magari ya Tesla, isipokuwa lenyewe limeongezewa ‘mbwembwe’ za hapa na pale na bei yake ipo chini ukilinganisha na magari ya Tesla.

 

Miongoni mwa ‘features’ zilizoongezwa, ni uwezo wa tairi za mbele na nyuma kukata kona! Yaani kama unavyoona tairi za mbele zinavyokata kona unapozungusha usukani, basi kuna kitufe kwenye ‘dash board’ ambacho ukikibofya, tairi za nyuma pia zinakata kona.

 

Sifa hii inaliwezesha gari kujiingiza na kujitoa kwenye ‘parking’ kwa ufanisi mkubwa, hata kama mbele kuna magari mengine. Na uzuri ni kwamba, ukifika mahali na ukataka kuliingiza kwenye ‘parking’, unashuka na kwa kutumia remote unaweza kulisogeza mahali popote unapotaka.

 

Ukitaka kuondoka pia huna haja ya kwenda mpaka kwenye parking, unabofya rimoti tu ambayo wakati mwingine inaweza kuwa simu yako, linajiwasha lenyewe, linajitoa kwenye parking na kusogea mpaka ulipo.

 

Lina ‘sensors’ zenye uwezo mkubwa wa kupima umbali yalipo magari mengine na kukadiria kama nafasi iliyopo inaweza kutosha kupita bila kuyagusa magari mengine! Mbali na teknolojia hiyo iliyoonesha kuwavutia wengi, pia ndani kuna ‘touch screen’ kubwa kwenye dashboard, ambayo inamsaidia dereva kuyajua mazingira ya nje ya gari vizuri bila kutazama kwenye ‘site mirrors’.

 

Yote tisa, kumi ni kwamba ndani ya gari kuna ‘sensors’ ambazo zina uwezo wa kutambua sura ya dereva, kwa hiyo kama ni mwizi anataka kuiba, sensors zikishindwa kumbaini tu, gari haliondoki, hata afanye nini.

 

Pia kuna sensors nyingine zinazoweza kutambua kiwango cha pombe alichokunywa dereva na kama kinavuka kiwango kinachotakiwa, gari haliwezi kuwaka mpaka pombe zipungue au aje dereva mwingine ambaye sura yake inatambulika na sensors.

 

Zipo sensors nyingine ambazo zinaweza kumbaini dereva anaposinzia akiwa anaendesha kisha kujibadilisha mfumo na kutoka ‘manual/automatic’ ambayo inategemea umakini wa dereva mpaka kwenye ‘self driving’, ambapo litakuwa likijiendesha lenyewe, ikishindikana, linajitoa barabarani na kujipaki, kisha linajizima.

 

Gharama yake ni Dola za Kimarekani 21,500 (takribani shilingi milioni 50) lakini linauzwa nchini China pekee wakati yale ya Tesla, gharama yake ilikuwa ni dola za Kimarekani 35,000 (takribani shilingi milioni 50).

Leave A Reply