The House of Favourite Newspapers

Yafaa Sasa Kubadili Mtazamo Wako Juu Ya Mapenzi

0

RAFIKI ni Ijumaa nyingine njema Mwenyezi Mungu ametujaalia.Tumeona wengi kwenye mapenzi wakiishi katika hali tofauti.

Wapo wenye pesa na wasionazo. Wapo wenye furaha na wasionayo. Yote hii inachangiwa na sababu nyingi ikiwemo wapenzi kujikuta wanaingia kwenye mapenzi wakisukumwa na sababu zisizo na msingi.

 

Ziko sababu nzuri za kuingia kwenye mapenzi. Nimejaribu kutafuta zile ambazo usipokuwa makini zitakutumbukiza shimoni na kujikuta ukijuta na kulia.Ukweli ni kwamba, uhusiano wa mapenzi unavunjika mno kwa sasa. Hali ya kiwango cha kumaanisha kwa wapenzi ni kudogo hivyo kushusha uthamani wa penzi.

 

Baada ya kusoma hapa, yafaa sasa kubadili mtazamo wako juu ya uhusiano wa kimapenzi.Kuingia kwenye uhusiano kwa lengo la kusaidiwa kiuchumi; hapa wengine wamewageuza wapenzi wao mitaji ya kuwaondoa kwenye umaskini.

 

Katika penzi la namna hii, hakuna muunganiko wa kuhisia baina ya wapenzi, bali kinachowaunganisha ni kile kilicho mfukoni. Athari za penzi la aina hii linafungua milango mingi kwa wahusika kutokuwa waaminifu.

 

Kuna hofu ya umri kupita na kuzeeka; katika kipengele hiki wapo wengi, hasa wanawake ambao wamejikuta wakiwakubali wanaume ilimradi tu nao waolewe maana umri umesonga hivyo hofu ya kutoolewa kutanda.Kuna suala la kuingia kwenye mapenzi kwa sababu ya mimba.

 

Lazima kutofautisha sababu iliyowafanya kuzaa mtoto kabla siyo itakayowafanya kuoana. Acha sababu ya kuoana kwenu iwe penzi lenu la dhati na siyo mimba.Kuna ishu ya kulazimika kuingia kwenye mapenzi ya kudumu kwa sababu ya upweke; hapa mara nyingi mtu anapokuwa peke yake (single) huwaza kuwa mapenzi ndiyo yanayoweza kuwa utatuzi wa matatizo yao.

 

Wapo wengine waliodhani mapenzi ni suluhisho la upweke waliokuwa nao na mara walipoingia humo, mawasiliano baina yao yakayumba hivyo kukomaza upweke.Kuolewa au kuoa kwa sababu ya shinikizo la wazazi, ndugu au marafiki; shinikizo kama hili linaweza kuwa la  ihisia au kihalisia.

 

Kihisia ni pale ndugu au wazazi wanapokushawishi kuoa kwa sababu umri unaonekana kukutupa mkono na wako wazazi wengine husisitiza kuwa wanataka wajukuu. Shinikizo kama hili ni pale wazazi wanapolazimisha watoto wao kuoa au kuolewa na watu fulani kwa sababu tu ni rafiki zao au kwa sababu ya kulinda utajiri.

 

Ndoa nyingi za aina hii zimekuwa kero na dimbwi la maumivu na machozi. Jiulizeni; unaingia kwenye mapenzi kwa furaha yako au wazazi?Kuamua kuoa au kuolewa ili kupata uhuru; hii hutokea kwa wale waliozoea kubanwa na wazazi katika kila wafanyacho.

 

Wengine huzikimbia familia zao maana hazieleweki, hazina mpangilio hivyo kutamani kutoka ili wakaanzishe za kwao. Akina dada na kaka wanachoka kuamuliwa na kuwekewa masharti ya kuvaa, kula, kufanya mambo, kutoka na kurudi kwa muda hivyo wanadhani kuingia kwenye mapenzi watajichomoa kifungoni.

 

Lengo la kuingia kwenye mapenzi, liwe zuri au baya ndilo litakalotengeneza aina ya maisha kuwa ya furaha au machungu.

 

Matokeo huwafanya wapenzi kuanza kutafuta kutoshelezwa nje ya uhusiano na hapo ndipo vinazaliwa vitu vingine kama uzinzi, kutengana, talaka au ugomvi.Kwa sababu ya kukosa maarifa; wengi hawajui wafanye nini ili kufanya mapenzi yao yawe imara.

 

Thamani ya penzi na jinsi linavyochukuliwa na watu wa karibu siku hizi ni tofauti na nyakati za wazazi wetu na hii imewafanya wengine kujikuta kwenye mapenzi kwa sababu mbovu hivyo uhusiano kuvunjika baada ya muda mfupi tu.

 

Lakini yafaa sasa kwa wapenzi kufahamu kwamba, mambo yamebadilika, zamani binti akikutwa bikra wakati anaolewa ilikuwa ni sifa kwake na familia nzima. Lakini siku hizi binti akikutwa ni bikra anachekwa na watu kumshangaa wakihisi ana matatizo fulani.

 

Kuwindana na kuchunguzana kumekuwa kawaida, maadili siyo jambo la kuzingatiwa tena na sasa wapenzi wengi wana majeraha moyoni, lakini yafaa sasa kubadili mtazamo wako juu ya mapenzi!Kwa leo ninaishia hapa, tukutane wiki ijayo.

NA Hashim Aziz +255 719401968

Leave A Reply