The House of Favourite Newspapers

Yafahamu Matukio 5 Ambayo Marekani Hawatayasahau

0

MAREKANI ni taifa kubwa kiuchumi linalotajwa kuwa taifa namba moja duniani lenye nguvu ya ushawishi kwenye maeneo mengi ikiwemo kijeshi, kisiasa na kiuchumi. Mara nyingi limekuwa mstari wa mbele kwenye kuchukua hatua ama maaamuzi yenye kugusa jamii kubwa.

 

Nguvu zake zimeifanya kuwa taifa lenye watu wengi wanaolipenda yakiwemo mataifa mbalimbali, lakini pia ni moja ya mataifa yanayochukiwa kutokana na maamuzi na wakati mwingine inavyotafsiriwa kuingilia utamaduni ama masuala ya nchi zingine.

 

Pamoja na hilo na kuwa na nguvu hizo, taifa hilo limekuwa likipitia misukosuko mingi iliyotikisa historia yake na kuacha kumbukumbu isiyofutika. Baadhi ya matukio yasiyosahaulika kwa Wamarekani ni haya matano.

5: Shambulio katika Ubalozi wa Marekani huko Tehran, Iran

Katika miaka ya 1970 kuliibuka vuguvugu la kiutawala baada ya vijana wengi wa nchi hiyo kuupinga utawala wa Mohammed Reza Shah Pahlavi.

 

Kukafanyika maandamano na ghasia katika maeneo mengi kuonyesha kuchoshwa na utawala wa kiongozi huyo aliyekaa kwa muda mrefu. Marekani imekuwa ikizozana na Iran kwa muda mrefu.

 

Julai 1979 alilazimika kuachia ngazi na kukimbilia Misri na Ayatollah Ruhollah Khomeini, aliyewaahidi uhuru zaidi watu wa Iran akaingia madarakani. Novemba 4, 1979, kundi la wanafunzi wa Iran lilivamia ubalozi wa Marekani ulioko Tehran, na kuteka zaidi ya Wamarekani 60.

Kwa nini waliamua kuteka Wamarekani?

Ni kwa sababu Rais wa Marekani wakati huo Jimmy Carter aliamua kuruhusu Shah kutibiwa ugonjwa wa saratani nchini Marekani. Hilo liliwaudhi sana Wairan.

 

Wanafunzi hao waliruhusu mateka wachache waliokuwa wagonjwa na Wamarekani weusi kabla ya kuwaachia mateka wote Januari 21, 1981, siku 444 baada ghasia kuanza na masaa machache baada ya Rais Ronald Reagan kuapishwa kuchukua nafasi ya Carter. Tukio hili halitoki kichwani mwa Wamarekani.

4: Shambulio la ubalozi wa Marekani mjini Beghanzi, Libya

Kushambuliwa kwa ubalozi wa Marekani nchini Libya ni pigo lingine ambalo limeitikisa Marekani. Ilikuwa Septemba 11 na 12 mwaka 2012, katika ubalozi huo uliokuwepo Benghazi, wapiganaji wa Kiislam walivamia usiku na kuendesha mashambulio yaliyosababisha vifo vya Wamarekani wanne akiwemo balozi wa Marekani nchini Libya.

 

Kifo cha Balozi huyo kilikuwa cha kwanza kilichotokana na ghasia ama kushambuliwa tangu mwaka 1988. Wapiganaji hao walikuwa sehemu ya Walibya waliokuwa wanataka mabadiliko lakini pia kupinga kuingiliwa kwa nchi hiyo na mataifa ya nje ikiwemo Marekani.

 

Balozi John Christopher aliteuliwa kuwa balozi mwezi mei 2012 akiwa kwenye ofisi za ubalozi mjini Tripoli lakini alienda Benghazi makazi ya mengine madogo ya balozi na wamarekani, kwa ajili ya shughuli maalumu kabla ya kukutwa na maswahibu hayo.

 

Usiku wa septemba 11, wanamgambo wa kiislam zaidi ya 150 wanaohusihwa na kundi la Al-qaeda walivamia na kushambulia na kuwasha moto kwenye jengo kubwa na kusababisha vifo vya wamarekani hao wanne, akiwemo Balozi.

3: Kuuawa kwa Rais John F. Kennedy

John Kennedy alikuwa rais wa 35 wa taifa hilo. Aliishi kifahari kwa kuwa alizaliwa kwenye familia ya kitajiri na ya wanasiasa huko Brooklyn, Massachusetts.

 

Kennedy alikuwa rais kuanzia mwaka 1961 mpaka 1963 alipouawa, lakini katika muda huo mfupi aliotawala, alionekana kuwa na ushawishi mkubwa na kuwa miongoni mwa vinara wa vita barini akielekeza nguvu zake nyingi kwenye mahusiano ya Muungano wa Soviet na Cuba.

 

Kifo chake kiliacha simanzi kubwa kwa Wamarekani, kwa sababu alikuwa anaonekana na dhamira ya kuleta maabadiliko makubwa nchini humo, ikiwemo mpango wake mkubwa wa kuuondoa utawala wa Rais Fidel Castro nchini Cuba, ulioonekana tishio kwa usalama wa Marekani.

 

Aliuawa Novemba 22, 1963 kwa kupigwa risasi huko Dallas, Texas na mtu aliyetajwa kwa jina la Lee Harvey Oswald, aliyekuwa mwanajeshi wa zamani wa majini. Oswald alitiwa nguvuni kwa kitendo hicho, lakini na yeye alitandikwa risasi na Jack Ruby siku mbili baadae.

2: Janga la Corona

Tangu kuibuka kwa janga anga la Corona mwishoni mwa mwaka 2019 limeathiri karibu mataifa yote ulimwenguni. Kuna visa zaidi ya milioni 220 vilivyoripotiwa ulimwenguni vifo vikivuka milioni 6.56.

 

Lakini athari kwa taifa la Marekani zimekuwa kubwa zaidi kutokana na na nchi hiyo kuwa na idadi kubwa ya visa vya korona vikifikia milioni 40.5 na vifo zaidi ya 662,000.

 

Uchumi wa Marekani umetikiswa na janga, hili na kufikia hatua ya tatizo la ajira kuwa kubwa kuwahi kutokea katika miongo kadhaa.

 

Kinachoisumbua Marekani kuhusu Korona ni kuongezeka kwa mzigo wa ajira. Kwa mujibu wa mtandao brookings, zaidi ya ajira milioni 20.5 zimepotea katika kipindi cha chini ya miaka miwili ya kuwepo kwa janga la korona.

 

Uzalishaji wa bidhaa na biashara haijawa sawa Marekani, tangu December 2019 na hilo linaifanya nchi hiyo kuwekeza nguvu zake nyingi kutoa chanjo ya corona kwa watu wake na kusaidia nchi zinazoendelea, ili kuliweka salama na kulirejesha katika nafasi yake.

1: Shambulio la Septemba 11, 2001

Tukio kubwa kuwahi kuitingisha Marekani ni tukio la kigaidi la Septemba 11, 2001 lililosababisha vifo vya vifo vya watu zaidi ya 3,000.

 

Washambuliaji wa kujitoa mhanga waliteka ndege nne za shirika la ndege la Marekani na kuzitumia kushambulia kwa kuzibamiza kwenye majengo makubwa mawili: Jengo la biashara la New York trade Center na jengo la Pentagon, makao makuu ya jeshi la Marekani.

 

Shambulio hili lililoacha zaidi ya majeruhi 10,000 limeisumbua Marekani kwa muda mrefu na kuamua kuendesha shughuli za kijeshi katika nchi za Iraq na Afghanistan na kufanikiwa kumuuua Osama Bin Laden kiongozi wa Al qaeda kundi linalotajwa kutekeleza mashambulizi hayo na kuuondoa utawala wa Saddam Hussein pale Iraq na utawala wa Taliban pale Afghanistan.

 

Miaka 20 ya kuhaha na makundi ya wapiganaji wa kiislamu likiwemo Al-qaeda linaloaminika kutenda shambuli hilo, Marekani imejiondoa katika nchi hizo, na kusababisha kurejea tena mamlakani.

Leave A Reply