The House of Favourite Newspapers

Yanga baba lao, inachapa tu

KWA matokeo ambayo Yanga inaendelea kuyapata katika mechi zake za Ligi Kuu Bara, ni sahihi kabisa kuwaita ‘baba lao’. Jana baada ya kuwachapa Mbao FC bao 2-0, sasa Yanga imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza.

 

Mechi pekee ambayo Yanga haijapata ushindi msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara ni dhidi ya watani wao wa jadi, Simba ambayo ilimalizika kwa suluhu wiki moja iliyopita. Lakini Yanga ipo mbele ya wapinzani wao hao Simba kwenye msimamo wa ligi, licha ya Wekundu kucheza mchezo mmoja zaidi. Yanga ina pointi 16, wakati Simba wana pointi 14.

 

Kama Yanga wakishinda mchezo wao mmoja wa kiporo, maana yake watakuwa wameiacha Simba kwa tofauti ya pointi tano. Yanga ilifanikiwa kupata bao dakika ya 16 likifungwa na kiungo fundi, Raphael Daudi aliyemalizia kwa kichwa faulo iliyopigwa na Ibrahim Ajibu.

Sasa Ajibu amefikisha jumla ya asisti sita katika mechi sita za ligi kuu ambazo Yanga imecheza. Heritier Makambo wa Yanga alikosa bao dakika ya 22 baada ya shuti lake la karibu kabisa na lango kudakwa na kipa wa Mbao.

 

Kipa Beno Kakolanya kwa mara nyingine alionyesha ubora baada ya kuokoa michomo kadhaa ya wachezaji wa Mbao, hasa dakika ya 22 ilipotokea piga nikupige kwenye lango lake lakini zote akaokoa. Dakika ya 24, Pastory Athanas alipiga shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari lakini mpira ukaishia mikononi mwa Kakolanya.

 

Mbao walionyesha kandanda safi katika mchezo huo lakini walishindwa kuzitumia vizuri nafasi walizotengeneza. Pastory alionekana kuwa mwiba mkali zaidi kwa mabeki wa Yanga na walilazimika kumchezea faulo za mara kwa mara ili kumpunguzia kasi. Kakolanya alitoka dakika ya 59 baada ya kuumia na kubebwa kwenye machela hadi vyumbani, na nafasi yake ilichukuliwa na Klaus Kindoki.

 

Ajibu alipiga bao la pili la Yanga dk ya 92 kwa tik tak safi ambapo mpira uligonga mwamba wa juu na kuzama wavuni. Yanga: Beno Kakolanya/ Klaus Kindoki dk ya 54, Paul Nyanganya, Gadiel Michael, Andrew Vicent/ Abdallah Shaibu ‘Ninja’ dk ya 74, Kelvin Yondani, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Deus Kaseke, Raphael Daudi, Heritier Makambo, Ibrahim Ajibu na Matheo Anthony/Thaban Kamusoko dk 53.

 

Matokeo ya mechi nyingine, Biashara United ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma, ilichapwa 0-2 na Mwadui FC shukurani kwa mabao ya Ibrahim Nasser (65) na Lameck Chamkaga aliyejifunga dk ya 89. JKT Tanzania ikiwa nyumbani ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Alliance. Abdulrahman Mussa aliifungia JKT (70) huku Juhudi Philimon akiifungia Alliance dk ya 90.

Ibrahim Mussa, Dar es Salaam

Comments are closed.