The House of Favourite Newspapers

Yanga Kupitisha Bakuli, Inaonekana Kiasi Gani Mmeishiwa Ubunifu

 

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaaya.

KLABU ya Yanga imetan­gaza kuanza kuchangi­sha fedha kwa ajili ya kujikwamua katika hali ngu­mu waliyonayo kipindi hiki.

 

Nilimuona Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaaya akiwaambia wanachama na wapenzi wa Yanga kwamba wanatakiwa kuacha kulaumu na badala yake mara moja kuanza kuichangia klabu yao ili kuhakikisha mambo yanak­wenda vizuri na wanajiondoa katika hali ngumu waliyonayo.

 

Katika kauli zake, Kaaya anawakumbusha wanacha­ma wa Yanga kuchangia kwa kuwa hali ni mbaya na wao wamekuwa wakilaumu tu la­kini sasa ni wakati wa wao kuonyesha mapenzi yao kwa vitendo.

Kama utaingia ndani ya kile ambacho amekuwa akikisema Kaaya, naweza kusema ni sa­hihi kabisa kwa wanachama na wapenzi wa Yanga kuonye­sha mapenzi yao kwa dhati.

 

Kuchangia klabu yao ni jam­bo sahihi kabisa na inatakiwa kuwa hivyo kwa kuwa ndiyo mapenzi ya dhati. Lakini kuna mengi kadhaa ya kujiuliza ambayo yalitakiwa kufanyiwa kazi au kutangazwa kabla ya michango ambayo wametaka wapewe na wanachama au mashabiki.

 

Moja, suala la michango ambayo iliwahi kuchangish­wa miezi kadhaa iliyopita na Klabu ya Yanga na mwisho ikaelezwa waliochanga wa­likuwa ni watu wachache sana, zilizopatikana ni kiasi gani? Na kama ni kiasi fulani, vipi zilitumika kufanyia nini? Na kama ni hivyo, msaada wa kile kidogo kilichopatikana, kiliisaidiaje Yanga?

 

Nauliza, baada ya wale wachache waliochanga, uon­gozi uliwashukuru? Pia wakati unaanza kuchangisha uliwa­kumbuka waliochanga wakati ule kwa kuwashukuru tena na kuwaomba msaada zaidi?

 

Haya yanaweza kuwa ni maswali ya awali ambayo tunaweza kujiuliza. Lakini kunaweza kuwa na mengi sana ya kujiuliza hasa kuanzia kwa Kaaya ambaye alikuwa akihusika na suala la masoko katika klabu hiyo.

 

Yanga ni ‘brand’ kubwa, vipi hadi sasa haina wadhamini wengi wa kutosha ambao wanaweza kuisaidia kufanya mambo yake vizuri.

 

Wale Macron ambao Yanga walieleza wataanza kuvaa jezi zao, tunajua ni kampuni kubwa kabisa. Vipi leo hakuna wanachoingiza ndani ya Yan­ga na kama kipo ni kiasi gani? Kwa kipindi hiki kimesaidia vipi, na kama hawapo, vipi wanachama au mashabiki ha­wajawahi kutangaziwa kama ilivyokuwa walitangaziwa ukionekana ni wakati mzuri na neema ndani ya Klabu ya Yanga?

 

Mchango kipindi hiki wakati ambao Yanga hawaaminiki na kuna maneno mengi yanazun­gumzwa wakituhumiwa kufuja baadhi ya fedha.

 

Wakati unawaomba wa­nachama na mashabiki michango lazima ufafanue, kwamba tuhuma zilikuwa hivi na vile. Mfano, Clement Sanga alielezea kuhusiana na matu­mizi yalivyokuwa baada ya kutuhumiwa, halafu akajiuzu­lu. Sanga hayupo tena.

 

Lakini bado kuna jambo am­balo Yanga walitakiwa kuli­fanyia kazi hasa na huenda lin­gewapunguzia kuanza kuomba michango. Hapa nazungumzia ada za wanachama wao ambao baadhi wamekuwa hawalipi.

 

Inaonekana wengi hawalipi ada zao, basi kupitia mata­wi yao lingefanyiwa kazi na kuisaidia klabu. Hata kama wangepata asilimia 60 ya madeni ya ada, ninaamini in­gesaidia kwa kiasi kikubwa.

Mwisho hata ule udhamini wa kampuni ya maji tunaouo­na kwenye matangazo ya Kla­bu ya Yanga, una faida? Yanga inalipwa kiasi gani.

 

Mwisho mwisho kabisa, namkumbusha Kaaya kuwa kuendelea kuomba misaada ni kukosa ubunifu kwa kuwa Yan­ga ina kila sababu ya kupata nafasi ya kujiendesha na ku­jiendeleza kwa fedha zake yenyewe na si kuomba.

 

Kipindi cha kutembeza ma­bakuli kwa klabu kama Yanga ni uvivu wa matumizi ya akili. Kinachotakiwa ni ubunifu zaidi na zaidi ili kupata wadhamini, kupata wanachama kwa wingi zaidi, kuingiza fedha nyingi za matangazo na kadhalika.

 

Najua haitakuwa rahisi, la­kini kama kiongozi unatakiwa kukutana na mambo magumu na kuleta mabadiliko. Kutaka vilaini ni kuonyesha uwezo mdogo hivyo, Yanga iachane na michango, viongozi wa­fanye kazi ya ziada kuikwamua klabu hiyo kwa ubunifu na mi­pango sahihi.

NA SALEH ALLY, HOJA YANGU, CHAMPIONI IJUMAA

Comments are closed.