The House of Favourite Newspapers

Yanga Mpya ya Mkwasa Kiboko

Mkwasa kiboko MABOSI wa Yanga tayari wana ripoti ya usajili ya dirisha dogo inayotaja nafasi za wachezaji inaotaka kuwasajili huku wakipanga kukutana na Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuisuka Yanga mpya.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu uongozi wa timu hiyo usitishe mkataba wa aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mkongomani, Mwinyi Zahera kwa kile kilichotajwa kutopata matokeo mazuri kwenye michezo ya michuano ya kimataifa.

 

Timu hiyo imepanga kufanya usajili bab’ kubwa katika usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 16, mwaka huu huku ikiacha baadhi ya wachezaji wakiwemo wa kimataifa na baadhi wanaotajwa ni Maybin Kalengo (Zambia), Issa Bigirimana (Burundi), Sadney Urikhob (Namibia) na Moustafa Selemani (Burundi).

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kutoka ndani ya Kamati ya Ufundi ya timu hiyo iliyopo chini ya mwenyekiti wake, Salum Rupia, wamepanga kukifanyia maboresho kikosi hicho kwenye nafasi nne muhimu.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa nafasi hizo walizopanga kuzifanyia maboresho ni safu ya ushambuliaji ambayo wamepanga kusajili washambuliaji wawili hatari wenye uwezo wa kufunga mabao akiwemo mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi, winga na kiungo mchezeshaji mmoja ambaye anatajwa Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.

 

Wengine ni beki wa pembeni namba tatu, tayari jina la Haji Mwinyi na beki wa timu ya taifa ya Rwanda, Erick Rutanga, beki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto ambao wanajadiliwa.

 

Aliongeza kuwa mara baada ya kamati hiyo kukutana na kocha huyo, watajua mapendekezo ya wachezaji anaowahitaji kusajiliwa akiwemo Niyonzima ambaye jina lake linatarajiwa kuwa la kwanza kujadiliwa baada ya Mwenyekiti wa timu hiyo, Dk Mshindo Msolla kukutana na kuzungumza naye huku akionyesha nia ya kurejea Jangwani.

 

“Kama unavyofahamu usajili wa dirisha dogo unakaribia hivyo ni lazima tuanze mapema mikakati ya kukiboresha kikosi chetu kwa kuanza kukutana na benchi la ufundi linalomshirikisha Mkwasa ambaye anakaimu nafasi ya kocha aliyekuwa kocha wetu ambaye ni Zahera.

 

“Hivyo, kama uongozi kamati yetu ya ufundi imepanga kukutana ndani ya wiki hii na Mkwasa ikiwa ni mapema kwa ajili ya kujadili masuala ya usajili na kati ya sehemu ambazo zinaonekana kufanyiwa maboresho katika kusajili ni ushambuliaji, beki wa kushoto ambaye yupo Haji ambaye mapendekezo makubwa yametolewa kwake.

 

“Pia kiungo mchezeshaji na Niyonzima ndiye anayetajwa kurejeshwa kikosini kwenye msimu huu ambaye ameonyesha nia kubwa ya kurejea Yanga na winga mmoja mwenye uwezo mkubwa wa kuanzisha mashambiulizi kwenye goli la wapinzani na yeye mwenyewe kufunga.

 

“Usajili ni lazima ufanywe, lipo wazi na uongozi umepanga kuungana na kocha kwa ajili ya kusimamia usajili wake, kufanyia kazi mapendekezo atakayoyatoa kwa wachezaji ambao anawahitaji katika kuisuka Yanga imara itakayoleta mataji ya ubingwa,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alizungumzia hilo kwa kusema: “Lipo wazi kabisa ni lazima usajili ufanyike katika dirisha dogo, tayari zipo baadhi ya nafasi ambazo hazihitaji kujadiliwa lazima tusajili, ikiwemo safu ya ushambuliaji, winga na beki.

 

“Kikubwa tunataka kuiboresha Yanga itakayoleta mataji ya ubingwa msimu huu, tunafahamu mashabiki wana kiu na timu yao kuona ikichukua ubingwa.”

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

 

 

Comments are closed.