The House of Favourite Newspapers

Yanga Ndiyo Tumeanza, Watuliza Mashabiki -Video

0

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima, jana Jumatano alirudisha furaha ndani ya kikosi hicho baada ya kufunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Gwambina FC.

 

Katika mchezo huo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la FA uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar, Yanga ilijipatia bao hilo dakika ya 45 ambapo Niyonzima alifumua shuti kwa mguu wa kushoto akiwa nje ya 18.

 

Yanga ambayo mara ya mwisho kupata ushindi ilikuwa Februari 8, mwaka huu uwanjani hapo ilipocheza dhidi ya Ruvu Shooting ukiwa mchezo wa Ligi Kuu Bara, ilicheza mechi nne mfululizo za ligi kuu na kuambulia sare, kabla ya kuibukia tena kwa Gwambina.


Mchezo wa jana ulijawa na hamasa kubwa ambapo wachezaji wa Yanga walijazwa ‘upepo’ na viongozi wao kwamba lazima washinde, wakashinda kweli.

 

Ushindi wa jana ulikuwa muhimu sana kwa Yanga ambao sasa wametinga robo fainali ya michuano hiyo sambamba na watani zao wa jadi, Simba.

Gwambina FC kwenye mchezo wa jana hawakuwa wanyonge kwani walifanya majaribio mawili makali ambayo yalipita juu kidogo ya lango la Yanga na kuwapa presha wapinzani wao.

 

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison, jana kama kawaida yake alizidi kuwa nyota wa mchezo kwa kutengeneza nafasi mbili ambazo wenzake walishindwa kuzitumia vema, huku akipiga pasi nyingi za uhakika.

 

Mara baada ya mchezo huo kumalizika, licha ya Yanga kuibuka na ushindi mwembamba, lakini mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakitamba kwamba: “Ndiyo tumeanza hivyo.” Wakimaanisha kwamba zile sare ni mwisho, sasa ni ushindi tu.

 

Timu zingine zilizofuzu robo fainali ya michuano hiyo ni Simba, Namungo, Sahare All Stars, Ndanda, Kagera Sugar, Azam na JKT Tanzania.

STORI NA MOLANDI, SPOTI XTRA

Leave A Reply