The House of Favourite Newspapers

Yanga: Tupeni Kombe Letu

0

Wilbert Molandi na Musa Mateja | CHAMPIONI| Dar es Salaam

NYOTA kadhaa wa Yanga wameapa kwamba, Simba ishinde au ifungwe mechi zake zilizobaki, ni lazima wao watwae ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kwani wamedhamiria kushinda mechi zote.

Straika Amissi Tambwe ametamka kwa kujiamini, kuwa Simba wafungwe, watoke sare au washinde lakini ubingwa wa ligi kuu ni lazima ubaki Jangwani.

Tambwe aliitoa jana Ijumaa asubuhi baada ya mazoezi yao ya mwisho kujiandaa na mechi yao ya leo ya ligi kuu dhidi ya Mbeya City itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa 10:30.

Kabla ya mechi ya jana ya Simba na Stand United, Yanga ilikuwa inaongoza ligi kuu ikiwa na pointi 62 sawa na Simba, inahitaji ushindi katika mchezo wa leo ili wajiweke katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya tatu mfululizo.

Ukiachana na mechi ya leo dhidi ya Mbeya City, mechi nyingine za Yanga ni dhidi Toto African na Mbao FC zote za Mwanza.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Tambwe alisema wao kikubwa wanachokiangalia ni kushinda mechi zote tatu walizozibakisha za ligi kuu ili kuhakikisha wanatwaa ubingwa.

Tambwe alisema; “Kama Simba  wanapiga hesabu za sisi kupoteza mechi zetu, basi wanajidanganya kwani tumejipanga vizuri kushinda.

“Hatutaki kuwaangalia Simba wanapata matokeo ya aina gani, washinde, wafungwe au watoke sare ni juu yao, sisi tumepanga kushinda mechi zote ili tuwe mabingwa.”

Winga wa Yanga, Simon Msuva yeye alisema: “Tumepania kushinda michezo yote iliyobaki ukiwemo wa kesho (leo) dhidi ya Mbeya City ili tuwe mabingwa.”

Naye Haruna Niyonzima alisema; “Napambana uwanjani ili niandike historia yangu ya kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo nikiwa na Yanga.”

Leave A Reply