The House of Favourite Newspapers

Yanga Yaanza ya Majembe Haya Dirisha Dogo

0

MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga na Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, amesema kuwa wamepokea ripoti ya usajili ya kocha mkuu wa timu hiyo, Mrundi Cedric Kaze, huku akiahidi kuifanyia kazi kwa kusajili wachezaji wote waliopendekezwa.

 

Wachezaji wanaotajwa kuwepo kwenye rada za Yanga katika usajili huu wa dirisha dogo ni Isah Ndala (Plateau United, Nigeria), Stephen Sey (Namungo), Meshack Abraham (Gwambina), Eric Rutanga (Polisi Rwanda) na Dack Kabangu wa DC Motema Pembe.

 

Kauli hiyo ameitoa mara baada ya dirisha la usajili kufunguliwa juzi Desemba 15, mwaka huu ambalo litafungwa Januari 15, mwakani kwa timu zote shiriki za ligi kuu na Daraja la Kwanza.

 

Yanga tayari imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji Mrundi Saidi Ntibanzokiza, ‘Saido’ ambaye tayari amejiunga na timu hiyo akisaini mkataba wa miaka miwili ya kukipiga Jangwani.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Hersi alisema kuwa tayari wanayo majina ya wachezaji yaliyokuwepo kwenye mipango ya usajili katika dirisha hili dogo wanayoendelea kuyafanyia kazi kwa kukamilisha taratibu za kuwasajili.

Hersi alisema kuwa wachezaji hao watawekwa wazi na kutambulishwa kwa waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha usajili wao kwani wapo baadhi wana mikataba, hivyo ni lazima wafuate taratibu za usajili kwa kuzungumza na klabu zinazowamiliki.

 

Aliongeza kuwa kikubwa wamepanga kufanya usajili wa kisasa utakaoendana na mahitaji ya kocha ikiwemo kusajili wachezaji watakaoingia kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja siyo kuanzia benchi.“

 

Tunafahamu dirisha la usajili limefunguliwa tayari na kama uongozi tumekabidhiwa ripoti ya usajili kutoka kwa kocha wetu Kaze ambayo ameomba mahitaji ya wachezaji katika baadhi ya sehemu kwenye kikosi chake.“

 

Hivyo kama uongozi tunaahidi kuifanyia kazi na kikubwa kama uongozi tuaahidi kuifanyia kazi ripoti hiyo kwa kusajili wachezaji wote aliowahitaji kocha kwani yeye ndiye anayefahamu upungufu wa timu yake bila ya kuingiliwa na mtu.“

 

Dirisha hili kocha ametoa mapendekezo ya kuwatoa kwa mkopo baadhi ya wachezaji wetu kwa ajili ya kwenda kulinda viwango vyao kati ya hao ni Mahadhi (Juma), Makame (Abdulaziz), Kiondo (Adam) na Fahad Omar,”alisema Hersi.

Leave A Reply