The House of Favourite Newspapers

Yanga Yabeba Viroba Vya Mchele Shelisheli

Kikosi cha timu ya Yanga.

YANGA wamepania kuvuka hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuitoa St Louis ya Shelisheli na imepanga kuondoka leo Jumapili ikiwa ‘full’ na viroba vya mchele kuepuka hujuma.

 

Jambo lingine ambalo Yanga imelifanyia kazi ni kununua viatu vya kuchezea katika matope kwani imepewa taarifa za wenyeji wao kuumwagia maji kwa makusudi Uwanja wa Linite watakaouchezea mjini Victoria, Shelisheli.

 

St Louis huwa wanatumia ujanja wa kumwaga maji hayo uwanjani ili uteleze huku wao wakiwa wamejiandaa na hali hiyo ili kuwapunguza nguvu wapinzani wao.

 

Katika mchezo wa awali, Yanga ilishinda bao 1-0 jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, hivyo St Louis wanajiandaa kushinda ili wasonge mbele katika raundi ya kwanza.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika, alisema: “Tuna mpango wa kwenda Shelisheli tukiwa tumekamilika.

 

“Tunakwenda na vyakula kutoka hapa nchini kufuatia kupewa ripoti na watu ambao wametangulia huko kwa ajili ya kuchunguza mambo mbalimbali.

 

“Timu itaondoka keshokutwa Jumapili kwa ajili ya kuelekea nchini Shelisheli kuwafuata wapinzani wetu St Louis, huenda tukabeba vyakula kutoka hapa nyumbani.”

 

Hata hivyo, Nyika alisema itategemea na ripoti ya mwisho ya watu ambao wapo tayari Shelisheli wakiendelea kuangalia mambo mbalimbali ikiwemo hali ya hewa, chakula na malazi.

Stori na Musa Mateja | Global Publishers

Comments are closed.