The House of Favourite Newspapers

Yanga Yakabidhiwa Majina Hatari ya Wabotswana

Kikosi cha timu ya Yanga.

TIMU ya Yanga, imepewa majina matatu ya nyota wanaokipiga kwenye kikosi cha Township Rollers ya Botswana ambao wanatakiwa kuwachunga ili wasiweze kuwaletea madhara watakapopambana katikati ya wiki ijayo. Jumatano ya wiki ijayo, Yanga inatarajiwa kucheza na timu hiyo katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Majina ya nyota hao watatu wanaokipiga kwenye kikosi cha Township Rollers ambayo inaongoza Ligi Kuu ya Botswana ni winga wa kulia Motsholetsi Sikele anayevaa jezi namba 28, kiungo wa kati Segolame Boy anayevaa jezi namba 11 (wote ni raia wa Botswana) na winga wa kushoto, Tshepo Matete, anayevaa jezi namba 18 ambaye ni raia wa Afrika Kusini.

 

Akiwazungumzia nyota hao, Rashid Mandawa ambaye ni straika Mtanzania anayekipiga kwenye kikosi cha BDF XI ya nchini humo, alisema: “Wapo wachezaji wengi tishio kutokana na timu yenyewe jinsi ilivyo, lakini wale wanaocheza nafasi za mbele kama Boy, Tshepo na Sikele ni hatari zaidi.

“Yanga wanatakiwa kufahamu kwamba wanakwenda kupambana na timu kubwa na wala wasiibeze kwani hapa Botswana, timu hiyo ina mashabiki wengi karibia nchi nzima wanaishabikia, kwa mashabiki tunaweza kusema ni kama ilivyo Yanga huko nyumbani. “Lakini pia tukizungumzia miundombinu ya timu, naifananisha Township kama Azam kwa maana kwamba ina uwanja wake kama ilivyo Azam vile, kwa ufupi hii timu inaendeshwa ki-profesheno zaidi.”

NA OMARY MDOSE

Comments are closed.