The House of Favourite Newspapers

Yanga Yapindua Meza Usajili wa Gadiel

MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Dk Mshindo Msolla amezungumzia mjadala wa usajili wa beki wa pembeni, Gadiel Michael na kutoa ruhusa ya mchezaji huyo kwenda popote atakapohitaji ikiwemo Simba inayotajwa kuwa mbioni kumsajili lakini beki huyo ni kama amepindua meza kibabe.

 

Kauli hiyo, ameitoa ikiwa ni siku moja tangu Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera kuwazuia mabosi wake kuendelea kumbembeleza beki huyo aliyegoma mara mbili kusaini mkataba mpya wa kubaki Yanga. Wakati Zahera na Msolla wakitoa kauli hizo, upande wa Gadiel naye alitua jana jijini Dar akitokea Misri alikokuwa na majukumu ya timu ya taifa na kufunguka kuhusu hatima yake katika mahojiano maalum na gazeti hili akionekana kuiweka Simba kapuni kwa muda.

Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Dk Mshindo Msolla.

Yanga na Gadiel Mara ya mwisho ni wiki iliyopita, Yanga kupitia mmoja wa mabosi wa klabu hiyo, alipanda ndege na kumpelekea mchezaji huyo mkataba akasaini akiwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichokuwa kinashiriki Afcon nchini Misri. Msolla ameliambia Championi Ijumaa kuwa, suala hilo lipo kwake hivi sasa na ataamua yeye asaini au asisaini, lakini kwao viongozi wamelifunga suala hilo.

 

Msolla alisema kuwa, hatasikitika kuondoka kwa beki huyo lakini atashangazwa na maamuzi yake atakayoyachukua ya kuchelewa kuwapa taarifa viongozi wa timu hiyo tangu awali kuwa anaondoka na badala yake kutafuta mchezaji mwenye hadhi na kiwango kikubwa cha kuichezea Yanga.

Aliongeza kuwa, kabla ya hayo kutokea yote beki huyo aliahidi na kuwathibitishia viongozi kuwa anabaki, hivyo wao waliachana na wachezaji wengi waliokuwa kwenye mipango ambao hivi sasa wamesaini timu nyingine. “Kiukweli kabisa Yanga wamepita wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa na waliocheza kwa mafanikio zaidi yake ambao nao wameondoka na kuiacha timu ikiendelea.

 

“Anachokifanya Gadiel ni kama kutaka kumsumbua mwajiri wake, siyo kitu kizuri hicho anachoendelea kukifanya, hivyo nimwambie kuwa hilo suala lake tumeshalifunga tayari na kilichobakia ni kuamua aondoke au abaki Yanga.

 

“Akitaka kusaini Yanga sawa, lakini nitasikitishwa na kitendo cha yeye kuondoka, pia nitakuwa nimejifunza kwa kupitia yeye kwa sababu atakuwa ametuchelewesha kupata mtu sahihi wa kuziba nafasi yake, licha kuwa na Sonso (Ally) lakini tulikuwa tunahitaji wawili wenye uwezo,” alisema Msolla.

 

Gadiel afunguka Mara baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jana mchana, Gadiel alizungumza kuhusu hatima yake kwa kusema: “Mimi bado nina mazungumzo na Yanga, ni timu yangu na wao ndiyo ninaowapa nafasi ya kwanza katika mazungumzo ya usajili wangu.

 

Alipoulizwa kuhusu tetesi za kusajiliwa na Simba, alisema: “Hizo ni tetesi tu, niamini mimi, muda huu naelekea Serena (hotelini) kwa ajili ya kuvunja kambi ya Stars kisha naenda kukutana na viongozi wa Yanga kuhusu hatima ya usajili wangu, nitafute baadaye nitakujulisha kitakachoendelea.”

Comments are closed.