The House of Favourite Newspapers

Yanga Yarudisha Milioni 112 Za Fei Toto Yajibu “Barua ya Mchezaji ina Dhana Potofu”

0
Rais wa Yanga SC, Mhandisi Hersi Said.

WAKATI taarifa zikieleza kwamba Kiungo wa Yanga, Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ ameandika barua ya kuvunja mkataba wake wa mwaka mmoja na nusu uliosalia ili ajiunge na Azam FC, klabu yake imebana kuzuia dili hilo.

Fei Toto ambaye alianza kuitumikia Yanga mwaka 2018, mkataba wake na klabu hiyo unatarajiwa kumalizika Mei 30, 2024.

Inaelezwa kwamba, Azam FC ambayo inamuwinda Fei Toto kwa muda mrefu, imemshawishi nyota huyo hadi kufikia kuandika barua ya kuvunja mkataba wake akilipa fedha za kufanya hivyo ili tu ajiunge nao.

Katika kujibu mapigo, jana Jumamosi, Yanga ilitoa taarifa ya ishu hiyo iliyoeleza kwamba: “Klabu ya Yanga, inaujulisha umma na wanachama wa Yanga kuhusiana na taarifa za mchezaji wetu, Feisal Salum Abdallah zinazoenea katika mitandao ya kijamii.

“Klabu inathibitisha kupokea barua kutoka kwa mchezaji tarehe 23 Disemba 2022 inayoeleza kuvunja mkataba baina yake na klabu.

“Klabu ya Yanga imemuandikia na kumjibu Feisal na miongoni mwa majibu ni kama ifuatavyo; Hakuna misingi ya kikanuni wala kisheria kulingana na mkataba wake ambazo zinampa haki mchezaji kusitisha mkataba wake na klabu kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wa sasa.

“Kanuni za taratibu za FIFA ziko wazi na zimeeleza taratibu zote juu ya jambo la aina hii. Kwamba mkataba baina ya mchezaji na klabu hauwezi kuvunjwa na upande mmoja tu bila kujadiliana na upande wa pili wakati msimu wa ligi ukiwa unaendelea.

Kiungo wa Yanga, Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’.

“Kwamba, kwa mazingira hayo, barua ya mchezaji ina dhana potofu na haina misingi ya kisheria ya kuvunja mkataba baina ya klabu na mchezaji.

“Na kwa mantiki hiyo, tumemuagiza Feisal azingatie matakwa ya mkataba wake kama ilivyoelezwa katika mkataba huo. Klabu pia imemkumbusha Feisal mkataba wake wa sasa ni halali hadi ifikapo tarehe 30, Mei 2024.

“Pamoja na hayo, tunapenda kuujulisha umma kuwa, kwa kuthamini kiwango na mchango wa Feisal kwa klabu yetu, tayari tulishaanza mazungumzo baina ya Klabu ya Yanga na wawakilishi wa Feisal wakiongozwa na mama mzazi wa mchezaji ili kuboresha maslahi yake na kuongeza muda wa mkataba wake wa sasa ambao unaisha Mei 2024.

“Hata hivyo, klabu haijapokea majibu mbadala wa mapendekezo ya maboresho haya kutoka upande wa Feisal na wawakilishi wake na badala yake tumepokea barua inayoelezea kuvunja mkataba kutoka upande wa Feisal ambayo ni kinyume na makubaliano ya mkataba wake wa sasa.

“Klabu tayari imesharejesha fedha kiasi cha TZS 112,000,000 (milioni mia moja na kumi na mbili) ambazo Feisal aliziweka katika akaunti ya klabu.

“Tunapenda kueleza kuwa, kuna utaratibu na kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na zile za Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ambazo ni lazima zifuatwe na timu yoyote ile inayotaka kumsajili mchezaji yeyote wa Klabu ya Yanga.

“Yanga inasisitiza kuwa, Feisal Salum Abdallah ni mchezaji halali wa Yanga na ana mkataba hadi kufikia Mei 30, 2024.”

 

STORI NA OMARY MDOSE

Leave A Reply