The House of Favourite Newspapers

Yanga Yategua Mitego ya Simba Kwa Nabi, Walipeleka Ofa Babu Kukwa Kwa Meneja Wake

0

MABOSI wa Yanga leo Jumatano jioni wanatarajiwa kufanya kikao kizito na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mtunisia, Nasreddine Nabi kwa ajili ya kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kukinoa kikosi hicho.

 

Championi Jumatano, linafahamu kuwa Simba ilimfuata meneja wa Nabi kwa ajili ya kufanya mazungumzo sambamba na kumpa dau nono ili akubali amrithi Mhispania, Pablo Franco.

 

Mabosi hao wa Simba walimpa ofa ya kumuongezea mshahara wake wa kila mwezi mara mbili kutoka Sh 20Mil anazochukua Yanga hadi 40Mil walizomuwekea mezani ili asaini mkataba.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, kutoka ndani ya Kamati ya Mashindano ya Yanga, leo mara baada ya mchezo wa Ligi Kuuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar mabosi na kocha huyo watakutana kufanya kikao cha kufikia muafaka wa kumuongezea mkataba.

 

Mtoa taarifa huyo alisema mabosi hao muda mrefu walimpa mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kukinoa kikosi hicho ambao hadi kufikia jana Jumanne mchana hakuwa ameusaini.

Aliongeza kuwa upo uwezekano mkubwa wa kocha huyo kusaini mkataba huo mwingine mpya baada ya kikao hicho kizito kitakachofanyika.

 

“Tunafahamu kila kitu kinachoendelea juu ya watani wetu (Simba) juu ya mipango yao ya kumtaka Nabi kwa ajli ya msimu ujao.

 

“Haitakuwa kirahisi kama wanavyofikiria kumchukua Nabi, hivyo kesho (leo Jumatano) uongozi utakutana na Nabi mara baada ya mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Mtibwa.

 

“Kikao hicho kitafikia muafaka mzuri na Nabi ikiwemo kusaini mkataba wa miaka miwili baada ya pande zote mbili kukubaliana na uzuri kocha mwenyewe ameonyesha nia ya kuendelea na Yanga baada ya kufarijika na mapokezi makubwa waliyoyapata baada ya ubingwa wa ligi kutoka kwa mashabiki,” alisema bosi huyo.

 

Nabi hivi karibuni alizungumzia hatima yake Yanga kwa kusema: “Mimi bado kocha wa Yanga na malengo yangu kuona nikiendelea nayo katika msimu ujao ambao tutacheza michuano ya kimataifa.”

Leave A Reply