The House of Favourite Newspapers

Yanga Yavunja Mwiko wa Tanzania Prisons, Sibomana Apiga Bonge Bao

0

PATRICK Sibomana jana aliwafanya mashabiki wa Yanga walale usingizi mnono kufuatia kufunga bao kali lililoipa ushindi wa bao 1-0 timu hiyo dhidi ya Tanzania Prisons.

 

Mechi hiyo ya ligi kuu ilipigwa Uwanja wa Uwanja wa Samora, Iringa hii ni baada ya awali kushindwa kufanyika Uwanja wa Sokoine, Mbeya kutokana na pichi ya uwanja huo kuharibiwa na wasanii waliokuwa na shoo.

 

Kabla ya mechi hiyo ya jana, Prisons ilikuwa ndiyo timu pekee ambayo haikuwahi kufungwa kwenye ligi msimu huu hivyo Yanga kupitia kwa mshambuliaji wake, Sibomana ambaye alitupia bao hilo dakika ya nne kiufundi wameweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo.

 

 

Sibomana alifunga bao hilo kiufundi akiunganisha juu kwa juu mpira uliorushwa na kiungo wa Yanga, Abdulaziz Makame kisha mwanaume akajiachia kwa shuti kali lililotinga kambani moja kwa moja akiwa ndani ya 18.

Katika mchezo huo, Yanga walionekana kuwa bora kwani walifanikiwa kutawala kipindi cha kwanza huku wakipigiana pasi mara kadhaa. Prisons walionekana kukamia mchezo huo lakini hadi mwisho hawakufanikiwa kupata bao.

 

Baada ya Sibomana kufunga bao hilo, dakika 12 baadaye almanusura beki Mustafa Seleman aifungie Yanga bao la pili kwa kichwa akiunganisha kona ya Sibomana lakini kipa wa Prisons, Jeremah Kisubi akaonyesha ufundi kwa kuokoa.Yanga waliendelea kuliandama lango la Prisons kupitia kwa Makame ambaye alikuwa gumzo katika mchezo huo kutokana na kurusha mpira miferu iliyosababisha madhara kwenye lango la Prisons.

Katika kipindi cha pili, timu zote zilifanya mabadiliko ili kuongeza nguvu lakini faida ilikuwa upande wa Yanga kwani waliendelea kulinda bao hilo na Prisons ambao walihaha kutaka kurudisha lakini wakishindwa kufanya hivyo.

 

Aidha katika mchezo huo ilishuhudiwa mchezaji wa Prisons, Idibily Buha akipata kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Mo Banka wa Yanga.

Kwa ushindi huo, Yanga wamefikisha pointi 21 katika michezo yao 10 waliyocheza na kupaa hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo huo ikiwa ni mara ya kwanza kushika nafasi tatu za juu tangu msimu huu umeanza. Mechi ijayo ya Yanga watacheza keshokutwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar dhidi Biashara ya Mara.

Leave A Reply