The House of Favourite Newspapers

Mastaa Hawa Wamefanya ‘Wandaz’ 2019

0

 

KILA mwaka unakuwa na maajabu yake kwenye maeneo mbalimbali. Kwa upande wa burudani hasa kwenye soko la Bongo Fleva, kuna maajabu mengi yamefanyika mwaka huu unaofikia ukingoni wa 2019.

 

Makala hii inaangazia orodha ya mastaa kumi (10) wa kike kwenye Bongo Fleva ambao wametusua kwa kufanya majaabu (wandaz) kwa mwaka huu 2019 kutokana na kazi zao, kuanzia ubora hadi mahali zilipofikia kwenye soko la muziki kimataifa.

 

V-MONEY

Hivi karibuni V-Money alitoa wimbo unaokwenda kwa jina la Never Ever ukiwa ni remix kwani alishawahi kuufanya kipindi cha nyuma. Awali, wimbo huu aliufanya kwa Prodyuza Nahreel wa The Industry na ulifanya vizuri mno. Wimbo huu aliamua kuufanya kitofauti huku akiwashirikisha wanamuziki maarufu duniani;

 

Frederic Gassita wa Gabon na The London Symphony Orchestra ambao ni washindi wa Tuzo za Grammy kwa miaka nane. Kwa kipindi chote cha mwaka huu, V-Money amefika mbali zaidi kimuziki kutokana na kazi zake kupigwa kwenye vituo vikubwa vya runinga nje ya nchi.

 

Wimbo wake mwingine wa Thats for Me uliweka rekodi baada ya kupigwa kwenye moja ya mechi za kikapu nchini Marekani (NBA), jambo ambalo si la kawaida kutokea kwa mwanamuziki wa Afrika.

 

NANDY

Nandy amefanya kazi kadhaa ambazo zimemsogeza sehemu nzuri kwenye soko la kimataifa. Nandy tunaweza kumhesabu kama mwanamuziki mwenye mafanikio makubwa zaidi akiwa na umri mdogo wa miaka 27 tu.

 

Mwaka huu Nandy alianza kufanya shoo zake mwenyewe zilizokwenda kwa jina la Nandy Festival ambazo alizifanya kwenye mikoa kadhaa nchini.

Shoo hizi ziliweka rekodi ya kujaza viwanja mbalimbali vya mpira mikoani. Mbali na hilo, alianza safari yake ya ‘kujiuza’ kimataifa baada ya kufanya kolabo kadhaa na Sauti Sol na Willy Paul wa Kenya.

 

MIMI MARS

Marianne Mdee, mwadada anayewakilisha vyema kutoka Lebo ya Mdee Music chini ya dada yake, Vanessa Mdee. Mwaka huu umekuwa wenye baraka tele kwake. Ameweza kufanya kazi ambazo zimemsogeza mbali kimuziki kama vile Ex, Mua na Ex Remix ambayo amemshirikisha MwanaFa.

 

Mbali na muziki, Mimi Mars amecheza filamu inayokwenda kwa jina la See You Again akiwa na waigizaji maarufu nchini Kenya na Afrika Kusini.

 

RUBY

Alikuwa kimya kwa kipindi kirefu, lakini mwaka huu alifanikiwa kurudi na kusumbua kiasi chake kutokana na kuachia kazi nzuri zilizofululiza na kumfanya kuwa na sura mpya kunako Bongo Fleva.

 

Ilishazoeleka kwamba, msanii anapokuwa kimya, huwa ni vigumu kurudi na kutusua kwani upepo unakuwa umebadilika, tofauti na walivyokuwa wanafanya kipindi cha nyuma.

Ngoma za Ruby ambazo ameziachia mwaka huu ni Alele, Ntade na Kelele ambayo ameshirikiana na mzazi mwenzake, Kusah.

 

GIGY MONEY

Ni mwaka wenye neema nyingi kwake kwani ameweza kufika mbali kutokana na kazi zake za muziki kukubalika na kupata madili ya kuwa balozi wa makampuni mbalimbali. Baadhi ya ngoma zake kwa mwaka huu ni pamoja na Changanya, Shoga na Usinisumbue.

 

LINAH

Kama ilivyokuwa kwa Ruby, naye alipotea kipindi fulani baada ya kujifungua, lakini mwaka huu amerudi na kufanikiwa kuachia ngoma kadhaa zilizomrudisha kwenye gemu. Kazi nzuri zilimfanya kupata shoo kwenye majukwaa makubwa ikiwemo Dubai na Afrika Kusini. Baadhi ya ngoma zake zilizofanya poa ni pamoja na Marry You, Umeniweza akiwa na Kayumba na Nimenasa akiwa na Amini.

 

MALKIA KAREN

Ameanza vizuri safari yake ya muziki. Kwa mwaka huu ameachia ngoma ambazo zote zimeweza kufanya vizuri ikiwemo Tutoke aliyoshirikiana na Rich Mavoko, Washa na Tabu ambayo mpaka sasa inatimiza wiki moja tangu aiachie.

 

JOLIE

Alikutwa na mtihani kidogo mwaka huu baada ya kumpoteza dada yake, lakini kwa msaada wa Mungu akaweza kunyanyuka na kufanya kazi nzuri. Ndiyo maana umeweza kumsoma kwenye orodha hii ya wasanii wa kike waliotusua mwaka 2019.

 

Jolie aliachia ngoma aliyoipa jina la Uoga ambayo imefanya vizuri kwa kukaa kwenye baadhi ya chati za muziki kwa muda mrefu. Pia ameachia ngoma ambayo mpaka sasa inatimiza wiki moja inayokwenda kwa jina la Sina ambayo nayo inakimbiza mitaani.

 

MAUA SAMA

Mwaka jana aliweza kuufunga na goma lake la kibabe ambalo lilikuwa likisumbua mno kutokana na ukubwa wake. Ngoma hiyo ilikuwa ni Iokote. Kwa mwaka 2019, ngoma hiyo imeendelea kusumbua kabla ya kudondosha mawe mengine kama Niteke ambayo baadaye alifanya Niteke Remix akiwa na Harmonize.

Makala: Ammar Masimba

 

Leave A Reply