The House of Favourite Newspapers

Yanga Yawapiga USM Alger ya Algeria Bao 2-1

YUSUF Manji amerudi na Yanga imeshinda dhidi ya Waarabu. Ndiyo, kikosi cha Yanga jana kiliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya USM Alger ya Algeria katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, mabao ya Yanga yalifungwa na Deus Kaseke dakika ya 43 na Heritier Makambo (47), huku lile la USM Alger likifungwa na Abderrahmane Meziane dakika ya 57.

Kabla ya mchezo huo, aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji aliwasili uwanjani hapo kutoa hamasa kwa wachezaji wa timu hiyo. Manji ambaye aliingia Uwanja wa Taifa majira ya saa 11 jioni, alianza kwa kusalimiana na mashabiki wa Yanga kabla ya kuingia kwenye vyumba vya wachezaji na kuzungumza nao kwa dakika kadhaa.

 

Yanga iliyopangwa Kundi D, katika mechi tano ilizocheza mpaka sasa, imepoteza tatu, sare moja, huku ikishinda moja. Imebakiwa na mechi moja dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda. Sasa imefikisha pointi nne katika kundi hilo, hivyo haiwezi kusonga mbele, na bado ipo mkiani. Ikumbukwe kuwa, Juni 15, 2016, Manji alitangaza kujiweka pembeni kwenye nafasi yake ya uenyekiti ndani ya Yanga, lakini Julai 13, mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia rais wake, Wallace Karia, lilitangaza kumtambua Manji kuwa ndiye mwenyekiti wa Yanga na haitambui kujiweka kwake kando.

Manji jana alionekana uwanjani akiwa pembeni ya Karia katika eneo la watu wazito, na baada ya mchezo huo, alirudi tena vyumbani kuzungumza na wachezaji akiambatana na mgeni rasmi wa mchezo huo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo.

Bado haijajulikana kama atakuwa tayari kuendelea na majukumu yake ya uenyekiti klabuni hapo. Katika mchezo wa jana, Makambo aligeuka gumzo kubwa kwa mashabiki ambao walikuwa wakiimba jina lake, na kuna wakati alipopiga shuti kali, mashabiki karibu wote wa Yanga walisimama kumpigia makofi.

 

Katika mchezo mwingine wa Kundi D, Gor Mahia ikiwa nyumbani ilifungwa 2-1 na Rayon Sport na kulifanya kundi hilo kuwa gumu. Gor Mahia ambayo bado inaongoza kundi ikiwa na pointi 8, inawania moja ya nafasi mbili ikiwa na USM Alger ambayo nayo ina pointi nane na Rayon ambayo ina pointi sita. Mechi za mwisho ni Agosti 29 ambapo ni Rayon Vs Yanga na USM Vs Gor Mahia. Rayon wanahitaji ushindi lakini Gor na USM zinaweza kusonga mbele kwa sare tu.

PICHA: RICHARD BUKOS, GPL

Comments are closed.