The House of Favourite Newspapers

Yondani atoka kifungoni, aanza na Lipuli FC

BEKI mkongwe na tegemeo wa Yanga, Kelvin Yondani, jana Alhamisi alimaliza adhabu yake na atarejea uwanjani
kwenye mchezo ujao dhidi ya Lipuli FC ya mkoani Iringa.

 

Yanga inatarajiwa kuvaana na Lipuli FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho utakaofanyika Jumatatu ijayo kwenye Uwanja wa Samora huko Iringa katika mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali.

 

Yondani atarejea uwanjani baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa michezo mitatu ya ligi huku akipigwa faini ya Sh 500,000 baada ya kupewa kadi nyekundu kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union.

 

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh amesema kuwa beki huyo alimaliza adhabu hiyo katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, hivyo kuanzia michezo ijayo ataanza kuonekana uwanjani. Saleh aliitaja michezo mingine ambayo aliikosa kuwa ni Mtibwa Sugar na Azam FC.

 

“Yondani ni mchezaji huru, ameyemaliza adhabu yake ya kufungiwa michezo mitatu. Hiyo ni habari njema kwa mashabiki wa Yanga katika kuelekea mchezo wetu na Lipuli kuwa beki wetu tegemeo amemaliza adhabu na atakuwepo katika mchezo huo,” alisema Saleh.

Comments are closed.