The House of Favourite Newspapers

Youssoufa Moukoko Kinda Tishio Duniani, Hadi Haaland Anamshangaa

0

MZALIWA wa Yaoundé nchini Cameroon aliyechukua uraia wa Ujerumani, Youssoufa Moukoko, wikiendi iliyopita aliweka rekodi ndani ya Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga.

 

Kijana huyo ambaye Ijumaa iliyopita ya Novemba 20 alitimiza miaka 16, Jumamosi akaweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kucheza mechi ya Bundesliga.

 

Ilikuwa ni dakika ya 85, mfungaji wa mabao manne kati ya matano ya Dortmund, Erling Haaland, anatoka na kumpisha Moukoko kuchukua nafasi yake, kijana ambaye amewashangaza wengi hadi sasa akiwemo Haaland.

 

Katika mchezo huo, Dortmund ikiwa ugenini iliibuka na ushindi wa mabao 2-5 dhidi ya Hertha Berlin. Moukoko, amevunja rekodi ya Nuri Sahin ambaye naye akiwa na kikosi hicho, aliweka rekodi ya kucheza Bundesliga akiwa na umri mdogo zaidi.

Miaka 16 na siku 335.

 

Ilikuwa Agosti 6, 2005. Rekodi za kijana huyo zinatisha sana kiasi cha Haaland ambaye naye yuko moto kwa kufunga na kuweka rekodi zake, anamshangaa, huku akiukubali uwezo wake na kumtabiria makubwa zaidi huko mbele. Tayari Moukoko amefunga mabao 141 katika mechi 88 akiwa timu za vijana za Dortmund ile ya chini ya miaka 16 na 19.

 

“Napenda kucheza sambamba naye. Nadhani ndiye kijana mwenye kipaji kikubwa zaidi duniani kwa sasa,” anasema Haaland na kuongeza.

 

“Ana miaka 16 na siku moja, ni kitu kizuri. Ana kazi kubwa ya kufanya mbele. Tuna bahati kubwa kuwa naye.” Tangu Agosti, mwaka huu, Moukoko alikuwa akifanya mazoezi na timu ya wakubwa ya Dortmund, lakini hakuwa na ruhusa ya kucheza kikosi cha kwanza kutokana na umri wake mdogo.

 

Wakati huo alikuwa bado hajafi kisha miaka 16. Sheria za Ujerumani, kama haujafi kisha miaka 16, huruhusiwi kucheza Bundesliga, hivyo Moukoko, akasubiri hadi wikiendi iliyopita kutimiza ndoto yake.

 

Msimu huu akiwa na kikosi cha vijana cha Dortmund chini ya miaka 19, tayari amefunga mabao 13 katika mechi nne. Katika mechi hizo, ana hat trick nne.

 

Kocha wa Dortmund, Lucien Favre, amemzungumzia kinda huyo akisema: “Kitendo cha kucheza kwake ni jambo zuri na timu kwa jumla. Bado ni kijana mdogo na hapa tuna nafasi nyingi za wachezaji kwenye eneo la ushambulia.

 

Tutaangalia itakuwaje, lakini kutokana na juhudi zake, anaweza kupata nafasi ya kucheza.” Kinda huyo mara ya kwanza anatua Dortmund, alijiunga na kikosi cha vijana chini ya miaka 16 wakati yeye akiwa na miaka 12. Msimu wa kwanza alifunga mabao 40, wa pili akafunga mabao 50.

 

Baada ya hapo, akapelekwa Dortmund U19 akiwa na miaka 14, hapo amecheza mechi 20 za ligi, amefunga mabao 34.

OMARY MDOSE

Leave A Reply