The House of Favourite Newspapers

Zahera Awanyatia Bocco, Kagere, Chama

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera.

 

MSIMU wa 2018/19 unaendelea na sasa hivi ndiyo mambo yanazidi kushika kasi, licha ya kuwa dirisha la usajili limeshafungwa, hilo halijazuia Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kutoa tamko juu ya wachezaji watatu wa Simba.

 

Ubora walionao nyota wa Simba, John Bocco, Meddie Kagere na Clatous Chama, umemfanya Zahera atoe tamko linaloonyesha anatamani kuwa nao kikosini kwake na kusisitiza kuwa kama hilo litatimia basi Yanga itatisha.

Zahera ambaye alianza kuinoa Yanga msimu huu, amefanikiwa kuiweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara timu hiyo ambapo kwa sasa ina pointi 50, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 40 na Simba pointi 33, ameonyesha wazi kuvutiwa na wachezaji hao wa wapinzani wao wa jadi.

 

Kocha huyo raia wa DR Congo, amesema siku Yanga ikiwa na uwezo wa fedha halafu akataka wachezaji kutoka Simba, basi moja kwa moja atawasajili Bocco, Kagere na Chama kukijenga zaidi kikosi chake ambacho anataka kukiona kikifanya vizuri ndani na nje ya Tanzania.

Zahera alisema Simba ina wachezaji wengi wazuri, lakini akiambiwa achague nani wa kusamjili kutokana na mahitaji yake, basi atawachukua nyota hao pekee na si wengine.

Akizungumza katika kipindi cha Nyundo ya Baruan Muhuza kinachorushwa kila Alhamisi saa 1:00 usiku kupitia Chaneli ya Azam Sports 2 iliyopo ndani ya King’amuzi cha Azam TV, Zahera, alisema: “Siwezi kuchukua wachezaji watano Simba, ila ukiniambia nichukue wachezaji kutoka kwao, ni wazi nitakuambia Bocco, Kagere na Chama, hawa jamaa ni wazuri.

 

“Mfano inatokea ninapata nafasi ya kuwasajili, watakuwa na msaada mkubwa kwenye timu yangu.” Katika hatua nyingine, Zahera baada ya kuiona Yanga ikiwa kwenye hali mbaya kiuchumi, ametoa mchongo ambao utaiingizia klabu hiyo takribani shilingi bilioni 45.

 

Zahera amesema, wakati hivi sasa Wanayanga wakiendelea kutembeza bakuli, yeye haoni sababu ya kufanya hivyo wakati kuna mtaji wa mashabiki wanaoweza kuchangia kwa utaratibu maalum na klabu ikanufaika.

 

Utaratibu huo ni ule wa kila shabiki kuchangia dola moja ambayo ni sawa na Sh 2,300, Yanga inaweza kuingiza si chini ya Sh bilioni 45 kwa muda mfupi.

 

“Yanga ina mashabiki karibu milioni 20, kila mmoja akitoa dola moja, basi klabu itapata dola milioni 20 (Sh bilioni 45), hiki ni kiasi kikubwa sana cha fedha katika uendeshaji wa timu, hatutakuwa na matatizo tena kuhusu fedha.

 

“Wapo mashabiki na wanachama wenye uwezo zaidi, hao wanaweza kutoa zaidi ya dola moja, hivyo hapo tutakuwa na fedha nyingi zaidi,” alisema Zahera.

Comments are closed.