The House of Favourite Newspapers

ZARI NOMA ANUNUA GARI LA KIFAHARI DUNIANI

DAR ES SALAAM: SHIKAMOO Zari! Ndivyo walivyoanza ‘kukomenti’ watu mitandaoni baada ya mwanamama mjasiriamali wa Kiganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kuonesha jeuri ya pesa kwa kununua moja ya magari ya kifahari duniani aina ya Rolls-Royce Ghost Black Badge la mwaka 2018, Ijumaa linakupa stori kamili.

 

Zari ameonesha jeuri hiyo juzi kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa SnapChat ambapo awali aliweka kipande cha video kinachomuonesha binti wake, Tiffah Dangote akiwa mbele ya gari hilo akiwa ameshika rimoti yake.

 

TIFFAH FULL KUBONYA…

Tiffah alianza kubonyeza rimoti hiyo ambapo kifaa maalum kilichopo mbele ya gari hilo kilichomoza kisha akabonyeza tena kikarudi ndani.

Baada ya hapo Tiffah akafungua milango yote ya gari hilo, akazama ndani. Tiffah alionekana akiingia na kukaa kwenye kiti cha dereva, akashika usukani na kurandaranda ndani ya gari hilo ambalo thamani yake inatajwa kuwa zaidi ya dola 350,000 za Kimarekani ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 821 za madafu.

AIBUA GUMZO

Baada ya kipande hicho kuanza kusambaa, gumzo la aina yake liliibuka mitandaoni ambapo mashabiki na wasiokuwa mashabiki wa mrembo huyo walianza kutoa maoni yao. Kuna ambao walipongeza kwa kitendo cha mrembo huyo kununua gari hilo la kifahari, lakini wengine waliponda kama ilivyo kawaida yao.

 

HOJA ZA WAPONDAJI

Kwa walioponda waliibuka na hoja kwamba gari hilo si lake bali ni la bwana mpya wa Zari ambaye naye anatajwa kuwa na ukwasi wa kutosha. “Hili gari si lake, litakuwa ni la yule bwana’ke mpya anayependa kumuita King Bae, Zari hana ubavu wa kununua gari kama hili ambalo tumezoea kusikia mastaa wa Marekani huko ndiyo wanamiliki,” alichangia mdau mmoja mtandaoni.

 

ZARI AWAJIBU

Baada ya maoni ya kuponda kuanza kuonekana kuwa mengi, Zari aliwatupia picha nyingine ya gari hilo kuonesha kwamba magari hayo yapo mawili na si moja kama baadhi ya mashabiki walivyodhani ambapo safari hii aliwawekea picha inayomuonesha yeye mwenyewe akiwa kwenye gari la aina hiyohiyo likiwa na utofauti mdogo sana wa rangi.

 

UPEPO WABADILIKA

Baada ya kuweka gari hilo, upepo kidogo ulibadilika na wale waliokuwa wanaponda kuonekana kuufyata kama si kuingia mitini kwani hawakuchangia tena mada.

NI KAMA NDEGE INAYOTEMBEA

Ndani ya gari hilo la Zari kuna siti zenye nafasi kubwa na zenye ubora wa hali ya juu ambapo katika siti wanazozitazama abiria wa nyuma, kuna skrini ndogo za kisasa zinazofunuka na kujifunika kwa kuongozwa na dereva au abiria aliyepanda.

 

Utulivu wa kwenye gari ni wa hali ya juu, kwani kwa namna lilivyoundwa si rahisi kusikia hata mashimo kirahisi hivyo kuwafanya abiria na dereva kuwa ‘comfortable’ wanapokuwa ndani hata kama litapita kwenye barabara yenye mashimo. Kama hiyo haitoshi, kuna kifriji kidogo katikati ya siti ya nyuma kwa ajili ya kupoozea vinywaji na eneo maalum la kuwekea glasi ambapo hata kuwe na mtikisiko si rahisi kudondoka.

 

MTAALAM WA MAGARI AFUNGUKA

Gazeti la Ijumaa lilizungumza na mtaalam wa kuuza magari aitwaye Abdulatif Shabaan, mkazi wa Ilala jijini Dar ambaye anauza magari tofauti ya kifahari, alilitaja gari kama hilo la Zari kuwa moja kati ya magari ya kifahari duniani.

 

Alisema japo magari hayo yanatofautiana kwa maana ya muundo na mwaka yaliyotengenezwa, lakini bado aina hiyo ya gari ndiyo inayokamata usukani kwa kuwa na magari ya kifahari duniani. “Rolls-Royce ndiyo aina ya magari yanayoongoza kwa magari ya kifahari duniani, sidhani kama hapa Bongo kuna mtu analo kama lipo basi ni kwa kuhesabu sana ila Sauz (Afrika Kusini) nafahamu yapo.

“Unajua haya Rolls-Royce yapo ya muundo tofautitofauti, kuna kama hilo la Zari ambalo ni Rolls-Royce Ghost Black Badge, kuna Rolls-Royce Phantom Black, Rolls- Royce Wraith, Rolls-Royce Dawn yaani kifupi yapo ya aina nyingi.

 

“Hapo utaangalia sasa yanatofautiana bei kutokana na mwaka yaliyotengenezwa. “Mfano hilo la Zari ni la mwaka 2018 ambalo linacheza kwenye shilingi bilioni moja kasoro hivi, lakini funga kazi ni Rolls- Royce Sweptail ambalo linacheza kwenye shilingi bilioni 30 za Kibongo,” alisema Abdulatif.

 

MAGARI MENGINE…

Aina nyingine ya magari ambayo yapo kwenye orodha ya magari ya kifahari duniani ni pamoja na Mercedes-Benz Maybach Exelero -Dola Milioni 8 (zaidi ya shilingi bilioni 18 za Kibongo), Koenigsegg CCXR Trevita – Dola 4.8 milioni (shilingi bilioni 11), Lamborghini Veneno Roadster –Dola 4.5 milioni (shilingi bilioni 10), McLaren P1 LM – Dola 3.6 milioni (shilingi bilioni 8) na Aston Martin Vulcan —Dola 3.4 milioni (shilingi bilioni 7).

 

ZARI KWELI NOMA

Historia inaonesha kuwa, mbali na Zari kumiliki mkoko huo wa maana, anayo magari mengine ya kifahari kama Lamborghini Gallardo, BMW-2006, Chrysler-2008, Audi Q7-2010, Hummer H2 na Ranger Rover Sports.

Comments are closed.