Zawadi Bora kwa Ndugu ni Bima ya Afya ya Jamii Iliyoboreshwa – HPSS
TIMU ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na HPSS Boresha Afya imetembelea Global Media Group iliyoko Sinza-Mori, jijini Dar es Salaam na kutoa elimu na kuhamisisha wananchi kuutumia msimu huu wa sikukuu kutoa zawadi ya Bima ya Afya ya Jamii kwa ndugu na jamaa zao.
Akizungumza katika kipindi cha Front Page kinachorushwa na +255 Global Radio, Dkt. Boniface Marwa, ambaye ni Mratibu wa Ugharamiaji wa Huduma za Afya wa Tamisemi, amesema Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (iChf) ni Bima ambayo itamwezesha mwananchi kutibiwa kuanzia kwenye zahanati mpaka hospitali za Rufaa za Mkoa kwa gharama ya shilingi elfu thelathini (30,000) tu.
Aliongeza kuwa huduma ambazo mwananchi atazipata kupitia Bima hiyo ni kupata ushauri wa daktari, vipimo vya maabara, vipimo vya picha (x-ray na ultra sound), huduma za matibabu ya macho (isipokuwa miwani au lensi bandia, au jicho bandia), dawa, kulazwa, kujifungua, huduma za kinywa na meno pamoja na upasuaji (mdogo na mkubwa) kuendana na mwongozo wa matibabu.